Marekani yamuwekea vikwazo rais wa Zimbabwe kwa ufisadi

Marekani ilisema viongozi nchini Zimbabwe wamekuwa wakipora rasilimali za umma kwa manufaa yao kibinafsi.

Muhtasari

•Marekani imemuwekea vikwazo Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa pamoja na maafisa wengine wakuu kwa ufisadi na ukiukaji wa haki za binadamu.

Image: BBC

Serikali ya Marekani imemuwekea vikwazo Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa pamoja na maafisa wengine wakuu kwa ufisadi na ukiukaji wa haki za binadamu.

Siku ya Jumatatu serikali ya Marekani ilisema viongozi nchini Zimbabwe wamekuwa wakipora rasilimali za umma kwa manufaa yao kibinafsi.

Hatua hii inafutilia mbali agizo la zamani la vikwazo vya serikali vilivyoanzishwa mwaka 2003 na kuwaweka watu 11 na mashirika matatu kwenye orodha ya kimataifa - mpango wa vikwazo wa Global Magnitsky.

"Shughuli hizi haramu zinasaidia na kuchangia mtandao wa uhalifu wa kimataifa wa hongo, magendo, na utakatishaji fedha unaosababisha umaskini kwa jamii nchini Zimbabwe, kusini mwa Afrika, na sehemu nyingine za dunia," ilisema taarifa.

Marekani pia ilikosoa kulengwa kwa mashirika ya kiraia na vikwazo vikali kwa shughuli za kisiasa.

Vilevile Rais Mnangagwa, Makamu wa Rais Constantino Chiwenga na mfanyabiashara Kudakwashe Tagwirei pia wamewekewa vikwazo.

Mkewe Bw Mnangaga, Auxillia Mnangagwa, pia amewekewa vikwazo kwa sababu "anarahisisha shughuli za mume wake za ufisadi".

Serikali ya Marekani ilisema tabia chafu ya baadhi ya watu na makampuni yenye nguvu zaidi nchini Zimbabwe inalingana na vitendo vya wakiukaji wakubwa zaidi wa haki za binadamu na watendaji wafisadi duniani.

Marekani ilihakikisha kwamba "vikwazo hivi vya watu binafsi na mashirika haviiathiri Zimbabwe au umma wake".

Serikali ya Zimbabwe haijazungumzia kuhusu madai hayo ya hivi punde lakini ilitupilia mbali vikwazo vya hapo awali kama sehemu ya njama za nchi za Magharibi kuleta mabadiliko ya kisiasa.