Uuzaji wa nyama wapigwa marufuku mjini Kampala

Hatua hiyo ni kama sehemu ya vikwazo vya kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa wa kimeta, unaoathiri wanyama.

Muhtasari

•Mamlaka ya wanyama nchini Uganda imeripotiwa kupiga marufuku uuzaji wa nyama katika mji mkuu, Kampala.

Image: BBC

Mamlaka ya wanyama nchini Uganda imeripotiwa kupiga marufuku uuzaji wa nyama katika mji mkuu, Kampala, kama sehemu ya vikwazo vya kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa wa kimeta, unaoathiri wanyama.

"Usafirishaji wa ng'ombe, mbuzi, kondoo, nguruwe na bidhaa zitokanazo na nyama zao, kupitia au ndani ya Mamlaka ya Mji Mkuu wa Kampala, Wilaya ya Kampala, ni marufuku hadi itakapotangazwa tena," Wizara ya Kilimo, Sekta ya Wanyama na Uvuvi ilisema katika barua iliyotajwa na vyombo vya habari kadhaa vya ndani.

"Masoko ya mifugo, sehemu za vichinjio, ikiwemo kunakouzwa nyama, viwanja vya kupakia na maonyesho ya wanyama katika wilaya nzima yanafungwa mara moja."

Barua hiyo ni ya tarehe 1 Machi lakini ilipokelewa na mamlaka ya Kampala siku ya Alhamisi, kulingana na ripoti za gazeti la kibinafsi la Daily Monitor.

Afisa mmoja wa jiji aliliambia gazeti hili kwamba watafanya kazi na mashirika mengine kutekeleza hatua za karantini, lakini vyombo vya habari vya ndani vinasema sehemu za kuuza nyama za jijini bado zinaendesha shughuli zake.

Ugonjwa unaoambukiza sana wa mguu na mdomo husababisha homa na malengelenge yenye uchungu ndani ya mdomo na chini ya kwato - na unaweza kusababisha kifo kwa wanyama wadogo.