Maafisa wa polisi visiwani Zanzibar wametangaza kuwakamata watu 12 kwa tuhuma za kukiuka utaratibu wa dini ya Kiislamu kwa kula mchana hadharani kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhan.
Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Abubakar Khamis Ally amesema kufuatia video iliyosambaa mitandaoni ikiwaonyesha baadhi ya watu katika eneo la viwanja vya mnazi mmoja Zanzibar kula hadharani wakati wa mchana wa Ramadhani, Jeshi hilo lilifanya msako na kuwakamata watu wapatao kumi na wawili wakiwa na vielelezo ambapo amesema wanaendelea na taratibu nyengine ili kuwafikisha Mahakamani.
Aidha ameyataja makosa mengine ni pamoja na unyang’nyi, Madawa ya kulevya na makosa mengine ambapo watuhumiwa wanashikiliwa na Polisi na wengine tayari wameshahukumiwa Mahakamani.
“Kama mlivyoona na kama mlivyosikia juzi juzi kulikuwa na watu walisemekana pale Mnazi Mmoja wanafanya uhalifu na kula hadharani, basi siku zilizofuata tulifanya msako na tuliweza kuwakamata hao kama ambavyo mmesikia na tulikamata takribani wanafika 10-12 na vielelezo vyao, kwa hiyo tunaendelea kukamilisha taratibu za upelelezi kabla ya kuwafikisha mahakamani,” alisema kamanda huyo.
Kisiwa cha Zanzibar kinatajwa kuwa na takribani asilimia 98 ya wakazi kuwa Waislamu na ambao ni wahafidhina kwa dini hiyo.