12 waliokamatwa na polisi Zanzibar kwa kula mchana wamsekana pia walikuwa wavuta bangi

Wiki jana, watu 12 walikamatwa na ikaripotiwa kwamba walitiwa mbaroni na polisi visiwani Zanzibar kwa kosa la kula mchana tena hadharani kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhan.

Muhtasari

• "Kilichofanyika ni kwamba oparesheni hiyo iliwakamata waliokuwemo na wasiokuwemo. Wavuta bangi na wengine ambao walikuwa wanakula mchana,” alisema.

CP Hamad Khamis Hamad.
CP Hamad Khamis Hamad.
Image: Screengrab

Kamishna wa polisi visiwani Zanzibar amefafanua kuhusu suala lililochukua nafasi kubwa kwenye vyombo vya habari ukanda wa Afrika Mashariki kufuatia taarifa za kukamatwa kwa watu Zaidi ya 10 kwa tuhuma za kula mchana kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhan.

CP Hamad Khamis Hamad ameeleza kwamba watu wlaiokamatwa kwa kudaiwa kula hadharani si tu walikamatwa kwa kosa hilo bali pia walikamatwa kwa matumizi ya dawa za kulevya aina ya bangi.

Hamad alisisitiza kwamba hakuna sheria inayozuia mtu kula mchana hadharani kando na sheria za Kiislamu na kutaka watu kuelewa kwamba chanzo cha kukamatwa kwa 12 hao kilikuwa matumizi ya bangi.

“Kimsingi niseme tu kwamba hakuna sheria inayokataza watu wasile mchana mwezi wa Ramadhan, ukiondoa sheria za dini ya Kiislamu. Tukio lile ambalo lilitokea, nilipokea klipu kutoka kwa kiongozi ambaye sitamtaja hapa, kuna vijana pale eneo la Mnazi Mmoja ambao walikuwa wanavuta bangi, bado ninao hiyo klipu,” CP Hamad alieleza.

“Kwa hiyo tulichokifanyaq nilitoa mimi maelekezo kwamba ifanyike oparesheni wale wavuta bangi wakamatwe. Maana bangi ni kosa la jinai. Hakuna sheria hapa Zanzibar inayohalalisha uvutaji wa bangi, kilichofanyika ni kwamba oparesheni hiyo iliwakamata waliokuwemo na wasiokuwemo. Wavuta bangi na wengine ambao walikuwa wanakula mchana,” alisema.

Wiki jana, vyombo vya habari viliripoti kuhusu kamishna huyo wa polisi ambaye alikuwa akitoa maelekezo kwamba vijana katika kisiwa cha Zanzibar waliokuwa wakila mchana tena hadharani watiwe mbaroni.