Mashtaka ya ufisadi dhidi ya makamu wa rais wa Malawi yatupiliwa mbali

Dk Chilima alikamatwa Novemba 2022 kwa madai kwamba alikubali pesa ili kutoa kandarasi za serikali. Alikanusha mashtaka.

Muhtasari
  • Makamu wa rais amefika mara kadhaa mahakamani tangu kukamatwa kwake, ingawa kesi ya msingi haikuanza.

Mahakama ya Malawi imefuta mashtaka ya rushwa dhidi ya Makamu wa Rais Saulos Chilima baada ya mwendesha mashtaka wa serikali kuwasilisha notisi ya kusitisha kesi hiyo. Hakuna sababu zilizotolewa za uamuzi huo.

Dk Chilima alikamatwa Novemba 2022 kwa madai kwamba alikubali pesa ili kutoa kandarasi za serikali. Alikanusha mashtaka.

Hatua ya hivi karibuni imezua maswali kuhusu jinsi serikali inavyoshughulikia mashtaka kuhusu madai ya ufisadi.

Kukamatwa kwa makamu huyo wa rais kulifuatia shutuma alizopokea ili kushawishi utoaji wa kandarasi kwa Xaviar Ltd na Malachitte FZE, kampuni mbili zinazohusishwa na mfanyabiashara wa Uingereza Zuneth Sattar.

Bw.Sattar pia alikanusha mashtaka dhidi yake.

Makamu wa rais amefika mara kadhaa mahakamani tangu kukamatwa kwake, ingawa kesi ya msingi haikuanza.

Siku ya Jumatatu, hakimu mfawidhi Redson Kapindu aliamuru kuachiliwa kwake mara moja akitaja jalada kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) alilolitoa Ijumaa iliyopita la "kusitishwa kwa mashtaka dhidi ya mshtakiwa kuhusiana na makosa matatu ya rushwa".

DPP sasa ana siku 10 kulieleza rasmi bunge sababu za uamuzi wa kufuta mashitaka dhidi ya makamu wa rais kama inavyotakiwa na katiba, Jaji huyo alisema.

Wakili wa Dk Chilima, Khumbo Soko, alieleza kufarijika kwa uamuzi wa kuwafutia mashtaka. "Kufikia sasa, hatujui sababu za kusitishwa, inatosha kusema ni bunge pekee ndilo lenye mamlaka ya kujua," shirika la habari la Reuters lilimnukuu akisema. Wakosoaji wa Rais wa Malawi Lazarus Chakwera wanasema hatua hiyo ni dalili zaidi ya ugumu kwake katika kupambana na madai ya ufisadi.