Watoto wauawa wakati bomu likianguka karibu na hospitali ya Sudan

Mapigano yamezidi hivi majuzi katika vita vya kuudhibiti mji huo.

Muhtasari

•Watoto wawili waliuawa na wengine kujeruhiwa baada ya bomu kuanguka karibu na hospitali ya watoto katika mji wa magharibi wa Sudan wa El Fasher.

•Tangu Ijumaa, wakaazi wameshuhudia makabiliano makali na kurushiana risasi.

Image: BBC

Watoto wawili waliuawa na wengine kujeruhiwa baada ya bomu kuanguka karibu na hospitali ya watoto katika mji wa magharibi wa Sudan wa El Fasher, shirika la Madaktari wasio na Mipaka-MSF limesema.

Mapigano yamezidi hivi majuzi katika vita vya kuudhibiti mji huo.

Ni kituo kikuu cha mwisho cha mijini katika eneo la Darfur ambacho kimesalia mikononi mwa jeshi.

Imekuwa ikipigana na Wanajeshi wa Rapid Support Forces (RSF) kwa zaidi ya mwaka mmoja, katika vita vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo vimesababisha vifo vya maelfu ya watu na kuwalazimisha mamilioni kutoka kwa makazi yao.

Jeshi limeweza kushikilia El Fasher lakini hali ya wasiwasi imekuwa ikiongezeka huku RSF ikiuzingira mji huo tangu katikati ya mwezi uliopita na kutishia kushambuliwa.

Tangu Ijumaa, wakaazi wameshuhudia makabiliano makali na kurushiana risasi, mwandishi wa habari wa kujitegemea katika jiji hilo aliambia BBC.

Wakati fulani usiku wa kuamkia Jumapili mlipuko mbele ya Hospitali ya Watoto ya Babiker Nahar inayoungwa mkono na MSF huko El Fasher "ulisababisha kuporomoka kwa paa la chumba cha wagonjwa mahututi na vifo vya watoto wawili wanaopokea matibabu hapo, pamoja na baadhi ya walezi", shirika la MFS lilisema katika taarifa fupi iliyotumwa kwa BBC.

Wagonjwa pia walijeruhiwa na wale ambao wangeweza kutafuta usalama walifanya hivyo katika hospitali nyingine, ambayo tayari ilikuwa imechukua watu 160 waliojeruhiwa siku ya Ijumaa.

Haijabainika ni nani aliyehusika na shambulio hilo.

Sehemu ya kusini ya jiji, ambayo hapo awali ilichukuliwa kuwa salama na kimbilio la watu waliohamishwa, imekuwa ikichomwa moto.