Mtu mmoja afariki baada ya ndege ya Singapore Airlines kukumbwa na msukosuko

Waziri wa Uchukuzi wa Singapore Chee Hong Tat alisema serikali itatoa msaada kwa abiria na familia zao.

Muhtasari
  • Mamlaka ya Thailand imetuma ambulensi na timu za dharura kwenye Uwanja wa Ndege wa Suvarnabhumi.

Abiria mmoja amefariki na wengine zaidi ya 30 kujeruhiwa baada ya ndege ya shirika la ndege la Singapore kutoka London kuelekea Singapore kukumbwa na msukosuko mkubwa.

Ndege hiyo aina ya Boeing 777-300ER iliyokuwa inaenda Singapore ilielekezwa Bangkok na kutua saa kumi kasoro robo kwa saa za ndani (08:00 GMT).

Ndege hiyo ilikuwa na jumla ya abiria 211 na wafanyakazi 18, shirika hilo la ndege lilisema katika taarifa yake.

"Singapore Airlines inatoa rambirambi zake za dhati kwa familia ya marehemu," ilisema.

Shirika hilo la ndege liliongeza kuwa linashirikiana na mamlaka ya Thailand kutoa usaidizi wa kimatibabu kwa abiria, na lilikuwa linatuma timu Bangkok kutoa usaidizi wowote wa ziada unaohitajika

Mamlaka ya Thailand imetuma ambulensi na timu za dharura kwenye Uwanja wa Ndege wa Suvarnabhumi.

Waziri wa Uchukuzi wa Singapore Chee Hong Tat alisema serikali itatoa msaada kwa abiria na familia zao.

"Nimehuzunishwa sana na tukio kwenye ndege ya Singapore Airlines SQ321 kutoka London Heathrow hadi Singapore," alichapisha taarifa kwenye mtandao wa Facebook.

Bado haijabainika ni nini hasa kilitokea kwenye ndege hiyo.