Diane Rwigara aondolewa kwenye kinyang'anyiro cha urais Rwanda

Tume ya uchaguzi ilisema Rwigara mbali na vitambulisho ghushi vya wafuasi wake pia alishindwa kuwasilisha hati ya rekodi ya uhalifu.

Muhtasari

• Katika uchaguzi uliopita mwaka 2017 pia Diane Rwigara alizuiwa kugombea urais kwa kile ambacho tume ya uchaguzi ilisema alishindwa kukidhi vigezo vya tume ya uchaguzi.

Mwanasiasa wa upanzani nchini Rwanda Diane Rwigara ametupwa nje ya kinyang’anyiro cha urais kwa kutotimiza vigezo vya Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo.

Kulingana na Mwenyekiti wa Tume hiyo Oda Gasinzigwa, Rwigara pamoja na kuwa na vitambulisho ghushi vya wafuasi wake pia alishindwa kuwasilisha hati ya rekodi ya uhalifu.

''Rwigara Shima Diane, badala ya hati ya rekodi ya uhalifu yeye aliwasilisha nakala ya kesi. Pia alitoa hati ya kuzaliwa badala ya hati ya kubainisha uraia wake wa asili kama inavyoombwa na tume ya uchaguzi.kuhusu saini za wafwasi wake zinazoombwa na tume ya uchaguzi,alikosa saini za watu angalau 12 walio na vitambulisho halali kutoka wilaya na ambao wako katika orodha ya wapiga kura wa wilaya hizo 8. Kadhalika katika wilaya 3 wafwasi wake walitumia vitambulisho ghushi,’’ alisema Bi Gasinzigwa.

Miongoni mwa wagombea 9 waliotaka kuwania kiti cha urais ni wagombea watatu tu waliotangazwa katika orodha ya muda iliyotolewa na tume ya uchaguzi ,akiwemo rais Paul Kagame atakayegombea muhula wa 4 madarakani.

Wengine ni mwenyekiti wa chama cha Green Frank Habineza na Philippe Mpayimana ambaye ni mgombe binafsi- Kwa ujumla watu 9 walikuwa wamewasilisha makaratasi wiki iliyopita wakitaka kuwania kiti cha urais- sita hawakuidhinishwa na tume ya uchaguzi.

Wiki iliyopita alipowasilisha makarasi ya kugombea urais Rwigara aliambia vyombo vya habari kuwa na matumaini ‘’mara hii atakubaliwa kugombea’’ kwa kile alichosisitiza kuwa ‘’hata nilizidisha idadi ya saini za wafwasi zinazohitajika

Kwa mjibu wa sheria ya uchaguzi kila mgombea katika uchaguzi mkuu anaombwa kupata saini za wafwasi 600 yaani wafwasi 20 kutoka wilaya 30 za Rwanda.

Katika uchaguzi uliopita mwaka 2017 pia Diane Rwigara alizuiwa kugombea urais kwa kile ambacho tume ya uchaguzi ilisema alishindwa kukidhi vigezo vya tume ya uchaguzi ikiwa ni pamoja na saini ghushi za wafwasi wake.

Uchaguzi wa mwaka huu ambao utafanyika tarehe 14 mwezi Julai huenda ukawa ni marudio ya uchaguzi wa mwaka 2017 ambapo Rais Kagame alichuana na Phillippe Mpayimana na Frank Habineza ambao hawakupata hata asilimia moja ya kura.