Ndege iliyombeba makamu wa rais wa Malawi yatoweka

Bw Chilima, mwenye umri wa miaka 51, amekuwa makamu wa rais wa nchi hiyo ya kusini mwa Afrika tangu 2014.

Muhtasari

•Ndege ya Jeshi la Ulinzi la Malawi "ilitoweka kwenye rada" baada ya kuondoka katika mji mkuu, Lilongwe, Jumatatu asubuhi, taarifa hiyo iliongeza.

•"Wananchi wataarifiwa kuhusu maelezo yoyote kuhusu hali hiyo ukweli unapothibitishwa," ofisi ya rais ilisema.

Image: BBC

Ndege iliyokuwa imembeba Makamu wa Rais wa Malawi Saulos Chilima na watu wengine tisa imetoweka, taarifa kutoka ofisi ya rais imesema.

Ndege ya Jeshi la Ulinzi la Malawi "ilitoweka kwenye rada" baada ya kuondoka katika mji mkuu, Lilongwe, Jumatatu asubuhi, taarifa hiyo iliongeza.

Rais aliamuru operesheni ya utafutaji na uokoaji baada ya maafisa wa anga kushindwa kuwasiliana na ndege hiyo.

Ilitakiwa kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mzuzu, kaskazini mwa nchi hiyo, baada ya saa 10:00 kwa saa za huko (11:00 BST)

Baada ya kuambiwa tukio hilo na kamanda wa Jeshi la Ulinzi, Rais wa Malawi Lazarus Chakwera amefuta safari yake ya kuelekea Bahamas.

"Wananchi wataarifiwa kuhusu maelezo yoyote kuhusu hali hiyo ukweli unapothibitishwa," ofisi ya rais ilisema.

Sababu ya kutoweka kwa ndege hiyo bado haijajulikana, Jenerali Valentino Phiri alimweleza Bw Chakwera. Moses Kunkuyu, waziri wa habari wa Malawi, aliiambia BBC kuwa juhudi za kutafuta ndege hiyo ni "kubwa".

Bw Chilima alikuwa akielekea kuiwakilisha serikali katika mazishi ya waziri wa zamani Ralph Kasambara, aliyefariki dunia siku tatu zilizopita.

Kabla ya taaluma yake ya kisiasa, alishikilia nyadhifa muhimu za uongozi katika kampuni za kimataifa kama Unilever na Coca Cola.

Bw Chilima, mwenye umri wa miaka 51, amekuwa makamu wa rais wa nchi hiyo ya kusini mwa Afrika tangu 2014.

Ameoa na ana watoto wawili.

Tutaendelea kukuletea taarifa zaidi kadiri tutakavyozipata.