Ndege ya Makamu wa Rais Malawi huenda ilianguka msituni, jeshi lasema

Wanajeshi wamekuwa wakifanya msako katika msitu wa Chikangawa katika juhudi za kuitafuta ndege hiyo.

Muhtasari
  • Saulos Chilima na wengine tisa walikuwa wakisafiri katika anga ya nchi hiyo Jumatatu asubuhi wakati ndege yao ilipotoweka kwenye rada za uwanja wa ndege.
Image: BBC

Ndege iliyokuwa imembeba makamu wa rais wa Malawi huenda iliaanguka kwenye msitu ulioko kaskazini mwa nchi hiyo, afisa mkuu wa kijeshi amesema.

Saulos Chilima na wengine tisa walikuwa wakisafiri katika anga ya nchi hiyo Jumatatu asubuhi wakati ndege yao ilipotoweka kwenye rada za uwanja wa ndege.

Ndege hiyo ya kijeshi, ilikuwa ikisafiri katika hali mbaya ya hewa.

Wanajeshi wamekuwa wakifanya msako katika msitu wa Chikangawa katika juhudi za kuitafuta ndege hiyo.

Katika mkutano na waandishi wa habari Jumanne, kamanda wa Jeshi la Ulinzi la Malawi Paul Valentino Phiri alisema ukungu umepunguza uwezo wa kuona msituni, na hivyo kutatiza juhudi za utafutaji.

Rais Lazarus Chakwera amesema misheni hiyo lazima iendelee hadi ndege hiyo ipatikane.

Aliwaambia Wamalawi katika hotuba yake Jumatatu jioni: "Ninajua kwamba sote tuna hofu na wasiwasi - mimi pia nina wasiwasi.

"Lakini nataka kuwahakikishia kwamba sitasaza rasilimali yoyote inayopatikana kupata ndege hiyo na ninashikilia kila matumaini kwamba tutapata manusura."

Hata hivyo, chama cha Dk Chilima, United Transformation Movement (UTM), kilisema “kimesikitishwa” na shughuli hiyo ya utafutaji.

Maafisa wa UTM walidai kuwa shughuli hiyo ilianza saa 15:00 kwa saa za huko (14:00 GMT) licha ya ndege kutoweka saa 10:00.

Makamu wa rais na rais wanatoka vyama tofauti lakini wawili hao waliungana kuunda muungano wakati wa uchaguzi wa 2020.

Dk Chilima (51) alikuwa akielekea kuiwakilisha serikali katika mazishi ya aliyekuwa waziri Ralph Kasambara aliyefariki siku nne zilizopita.

Mke wa Rais wa zamani Shanil Dzimbiri pia alikuwa kwenye ndege hiyo, iliyopaa kutoka mji mkuu, Lilongwe, Jumatatu asubuhi.