Hospitali za siri zinazowapa wahalifu sura mpya

Hospitali mbili kama hizo zitafungwa "katika wiki zijazo" baada ya polisi kuvamia hospitali ya kwanza.

Muhtasari

•Vifaa vya kupandikiza nywele, vipandikizi vya meno na dripu za IV za kung'arisha ngozi zilinaswa katika hospitali ya Pasay City miezi miwili iliyopita.

•"Zinaonekana kama kliniki za kawaida kwa nje, lakini ukiingia, utashtushwa na aina ya teknolojia waliyo nayo," Bw Casio alisema.

Image: BBC

Hospitali za siri nchini Ufilipino zimekuwa zikitoa huduma za upasuaji wa kubadili sura kwa wakimbizi na matapeli ili kuwasaidia kukwepa kukamatwa, mamlaka zinasema.

Hospitali mbili kama hizo haramu zitafungwa "katika wiki zijazo" baada ya polisi kuvamia hospitali ya kwanza katika vitongoji vya kusini mwa Manila mwezi Mei, msemaji wa polisi aliambia BBC.

Vifaa vya kupandikiza nywele, vipandikizi vya meno na dripu za IV za kung'arisha ngozi zilinaswa katika hospitali ya Pasay City miezi miwili iliyopita.

"Unaweza kuunda mtu mpya kabisa hapa," alisema Winston John Casio, msemaji wa Tume ya Rais ya Kupambana na Uhalifu uliopangwa (PAOCC).

Hospitali hizo mbili haramu zilizo chini ya uangalizi zinaaminika kuwa kubwa mara nne kuliko ile ya Pasay, mamlaka ilisema.

Wateja wao wanadaiwa kujumuisha wacheza kamari mtandaoni, ambao wanaendesha shughuli zao nchini Ufilipino kinyume cha sheria, Bw Casio alisema.

Kamari za mtandaoni au Pogos huwadumia wachezaji wa China Bara, ambapo kamari ni kinyume cha sheria.

Lakini polisi wanasema Pogos zimetumika kuficha shughuli za uhalifu kama vile ulaghai wa simu na biashara ya binadamu.

Madaktari watatu - wawili kutoka Vietnam na mmoja kutoka China - mfamasia wa China, na muuguzi wa Kivietinamu walikamatwa katika msako wa Pasay, ambao hakuna hata mmoja wao aliyepewa leseni ya kufanya kazi nchini Ufilipino.

Mamlaka pia ilipata mashine ya kusafisha damu, na kupendekeza kuwa kituo hicho, ambacho kilikuwa na ukubwa mita 400 mraba, kilitoa matibabu mbalimbali pamoja na upasuaji wa urembo.

"Zinaonekana kama kliniki za kawaida kwa nje, lakini ukiingia, utashtushwa na aina ya teknolojia waliyo nayo," Bw Casio alisema.

"Hospitali hizi za Pogo haziulizi vitambulisho vinavyofaa... Unaweza kuwa mkimbizi, au unaweza kuwa mgeni haramu nchini Ufilipino," alisema.

Mamlaka ilidokezwa kuhusu kuwepo kwa hospitali hiyo haramu katika Jiji la Pasay. Pogos ilistawi chini ya rais wa zamani Rodrigo Duterte, ambaye alitafuta uhusiano wa kirafiki na China wakati wa muhula wake wa miaka sita uliomalizika mnamo 2022.

Hata hivyo, mrithi wake Ferdinand Marcos Jr ameanzisha msako dhidi ya Pogos, akitaja viungo vyao vya uhalifu.

"Rais hataki Ufilipino ipakwe tope kama 'kitovu cha utapeli' na ametupa agizo la kusaka maeneo ya ulaghai kwa sababu ya jinsi yamekuwa yakilenga idadi kubwa ya watu kutoka kote ulimwenguni,"

Bw Casio alisema. Mnamo Desemba 2022, maafisa wa uhamiaji walimkamata mshukiwa wa genge la uhalifu kutoka China ambaye alidaiwa kufanyiwa upasuaji wa wa kubadili sura ili kuficha utambulisho wake.

Visa kama hivyo vinaweza kuhusishwa na hospitali ambazo hazijaidhinishwa Bw Casio alisema.