Bunge la Bangladesh limevunjwa, kwa mujibu wa taarifa kutoka ofisi ya rais.
Ilikuwa moja ya masharti yaliyotolewa na waratibu wa maandamano ya wanafunzi, ambao walikuwa wameweka makataa ya saa tisa (09:00 GMT).
Waandamanaji wa wanafunzi wamesema hawatakubali serikali inayoongozwa na jeshi, wakiongeza kuwa mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel Muhammad Yunus amekubali kuwa mshauri mkuu wa serikali ya mpito.
Huku hayo yakijiri Chama cha Huduma ya Polisi ya Bangladesh (BPSA) kimesema kuwa maafisa wake wameanza mgomo.
"Hadi usalama wa kila polisi utakapopatikana, tunatangaza mgomo," Mamlaka hiyo ilisema katika taarifa.
BPSA ambayo inawakilisha maelfu ya maafisa wa polisi kote nchini. Ilisema kuwa zaidi ya vituo 450 vya polisi vilishambuliwa siku ya Jumatatu, katika maandamnao ya kumshinikiza Waziri Mkuu Sheikh Hasina kujiuzulu.
Maafisa kadhaa wa polisi pia waliuawa wakati wa maandamano hayo, kulingana na maafisa.
Idhaa ya BBC Bangla tayari ilikuwa imeripoti kuwa hakuna polisi wa trafiki wanaoonekana kwenye barabara nyingi katika mji mkuu wa Dhaka mapema Jumanne, huku wanafunzi wakionekana katika baadhi ya maeneo wakielekeza trafiki.