Shangwe nchini Bangladesh baada ya Waziri Mkuu kuikimbia nchi

Bi Hasina, 76, alikimbia nchi, akiripotiwa kutua India siku ya Jumatatu.

Muhtasari

•Waziri Mkuu wa Bangladesh Sheikh Hasina amejiuzulu baada ya wiki kadhaa za maandamano mabaya dhidi ya serikali.

•Mjini Dhaka siku ya Jumatatu, polisi na majengo mengine ya serikali yalishambuliwa na kuchomwa moto.

Image: BBC

Waziri Mkuu wa Bangladesh Sheikh Hasina amejiuzulu baada ya wiki kadhaa za maandamano mabaya dhidi ya serikali, na kukomesha zaidi ya miongo miwili ya kutawala siasa za nchi hiyo.

Bi Hasina, 76, alikimbia nchi, akiripotiwa kutua India siku ya Jumatatu.

Umati wa watu walioshangilia walijitokeza barabarani kusheherekea taarifa hizo, huku wengine wakivamia ikulu ya waziri mkuu, wakiripotiwa kupora na kuharibu sehemu za makazi yake ya zamani.

Saa chache baada ya Bi Hasina kujiuzulu, Rais Mohammed Shahabuddin aliamuru kuachiliwa kwa waziri mkuu wa zamani Khaleda Zia aliyefungwa jela na wanafunzi wote waliokuwa wamezuiliwa wakati wa maandamano ya hivi karibuni dhidi ya mfumo wa upendeleo wa nafasi za kazi serikalini.

Rais Shahabuddin alisema alikuwa ameongoza mkutano wa wakuu wa jeshi na wawakilishi wa kisiasa.

Alisema serikali ya mpito itaundwa, uchaguzi mpya utaitishwa na amri ya kutotoka nje ya kitaifa kuondolewa.

Mjini Dhaka siku ya Jumatatu, polisi na majengo mengine ya serikali yalishambuliwa na kuchomwa moto.

Waandamanaji walijaribu kubomoa sanamu ya kiongozi wa uhuru Sheikh Mujibur Rahman, baba yake Bi Hasina.

Vikosi vya jeshi na polisi vilisambazwa katika jiji lote. Huduma ya simu za mkononi iliripotiwa kukatika kwa saa kadhaa kabla ya kurejeshwa.

Siku ya Jumatatu, waandamanaji walionekana wakibeba samani kutoka kwenye makazi ya waziri mkuu.

Makumi waliripotiwa kuuawa siku ya Jumatatu, ingawa idadi kamili bado haijafahamika. Shirika la habari la AFP liliripoti idadi ya waliofariki kuwa 66, ingawa shirika la habari la Dhaka Tribune lilisema kuwa watu 135 wameuawa.