Marekani yamkamata raia wa Pakistani anayedaiwa kutaka kumuua Trump

Mkurugenzi wa FBI Christopher Wray aliuita mpango huo "njama hatari ya kuua kwa malipo..

Muhtasari

•Asif Merchant, mwenye umri wa miaka 46, anashtakiwa kwa kujaribu kuajiri mshambuliaji huko New York ili kuwaua maafisa mashuhuri wa Marekani.

Image: BBC

Mwanaume mmoja raia wa Pakistani mwenye uhusiano na Iran ameshtakiwa kwa madai ya njama ya kumuua Donald Trump na wanasiasa wengine wa Marekani.

Mkurugenzi wa FBI Christopher Wray aliuita mpango huo "njama hatari ya kuua kwa malipo..

Asif Merchant, mwenye umri wa miaka 46, anashtakiwa kwa kujaribu kuajiri mshambuliaji huko New York ili kuwaua maafisa mashuhuri wa Marekani.

CBS, mshirika wa habari wa BBC, alinukuu vyanzo vikisema kuwa Trump alikuwa miongoni mwa walengwa.

Usalama wa mgombea huyo wa kiti cha urais wa chama cha Republican uliimarishwa mwezi Juni baada ya mamlaka kubaini kuhusu njama ya Iran ya kumuua.

"Njama iliyoelekezwa nje ya nchi ya kumuua afisa wa umma, au raia yeyote wa Marekani, ni tishio kwa usalama wa taifa letu na itakabiliwa kwa nguvu na rasilimali zote za FBI," Bw Wray alisema Jumanne.

Bw.Merchant alikamatwa mwezi Julai na anazuiliwa mjini New York. Kulingana na mashtaka ya wizara ya sheria, Bw Merchant aliwasili Marekani kutoka Pakistan mwezi Aprili baada ya kukaa kwa muda nchini Iran.

Baada ya kufika, inadaiwa aliwasiliana na mtu ambaye aliamini angeweza kusaidia mpango wa mauaji.

Inadaiwa kuwa Bw Merchant alimwambia mtu ambaye alipanga kuondoka Marekani kabla ya walengwa kuuawa, na kwamba angewasiliana kwa kutumia maneno ya siri.

Mshukiwa alimtaka mhusika kupanga mkutano na wauaji, hati ya mashtaka inasema.

Inadaiwa Bw Merchant aliwaambia maafisa hao kwamba walipaswa kuiba nyaraka kutoka kwenye nyumba ya mtu aliyelengwa, kupanga maandamano katika mikutano ya kisiasa, na kumuua "mwanasiasa".