Ndege moja imeanguka katika jimbo la São Paulo nchini Brazil na kuwaua watu wote 61 waliokuwa wameiabiri.
Ndege hiyo ya injini mbili ilikuwa safarini kutoka Cascavel katika jimbo la kusini la Paraná kuelekea uwanja wa ndege wa Guarulhos katika jiji la São Paulo ilipoanguka katika mji wa Vinhedo, shirika la ndege la Voepass linasema.
Kanda za video zinazosambazwa katika mitandao ya kijamii zinaonyesha ndege ikizunguka na hatimaye kuanguka.
Ndege hiyo aina ya ATR 72-500 ilikuwa na abiria 57 na wafanyakazi wanne.
Rais wa Brazil, Luiz Inácio Lula da Silva, ametuma rambi rambi zake kwa familia na marafiki wa waathiriwa.
Gavana wa jimbo la São Paulo, Tarcísio Gomes de Freitas, ametangaza siku tatu za maombolezo.
Ndege hiyo ilianguka katika eneo la makazi lakini hakuna mtu aliyejeruhiwa.