Iran ilihusika na udukuzi wa hivi majuzi wa kampeni za urais za Donald Trump, maafisa wa kijasusi wa Marekani wamethibitisha.
FBI na mashirika mengine ya shirikisho yalisema katika taarifa ya pamoja kwamba Iran imechagua kuingilia uchaguzi wa Marekani "ili kuchochea mifarakano na kudhoofisha imani kwa taasisi zetu za kidemokrasia".
Maafisa wa Kampeni ya Trump waliinyooshea kidole Iran tarehe 10 Agosti kwa kudukua jumbe zake za ndani. Maafisa wa Iran walikanusha.
Vyanzo vinavyofahamu uchunguzi huo viliiambia kampuni ya habari mshirika wa BBC wa Marekani, CBS News, kwamba wanashuku kuwa wavamizi wa kitandao wa Iran pia waliilenga kampeni ya mgombea urais wa chama cha Democratic Kamala Harris.
"[Jumuiya ya kijasusi] ina imani kwamba Wairani kupitia uhandisi wa kijamii na juhudi zingine walitafuta ufikiaji wa taarifa za watu binafsi wenye uwezo wa moja kwa moja wa kampeni za Urais za pande zote mbili za kisiasa," maafisa wa ujasusi wa Marekani walisema katika taarifa hiyo.
"Shughuli kama hizo, ikiwa ni pamoja na wizi na ufichuzi, zinalengo la kuathiri mchakato wa uchaguzi wa Marekani."
Bado haijulikani ni habari gani, ikiwa zipo, ziliibiwa wakati wa udukuzi. Trump alisema wadukuzi hao waliweza tu kupata taarifa zinazopatikana kwa umma.