Mwanamume mmoja amehukumiwa kifungo cha zaidi ya miaka sita jela baada ya kudukua hifadhidata ya serikali ili kughushi kifo chake, na kujiondoa kwenye mpango wa kulipia malipo ya gharama za mtoto.
Jesse Kipf kutoka Kentucky, nchini Marekani, alihukumiwa kifungo cha miezi 81 kwa ulaghai wa kompyuta na wizi wa utambulisho.
Mwanamume huyo mwenye umri wa miaka 39 alikiri kuingia kwenye Mfumo wa Usajili wa Kifo wa Hawaii mnamo Januari mwaka jana na kujiwekea taarifa zinazoonyesha kwamba alifariki dunia.
Kisha Kipf akajaza sehemu ya maombi ya kupata Cheti cha Kifo katika Jimbo la Hawaii, na kujiwekea sahihi kama mthibitishaji wa matibabu akijithibitishia kifo chake kwa kutumia sahihi ya dijiti ya daktari.
Ilimaanisha kuwa alifanikiwa kusajiliwa kama mtu aliyefariki dunia katika hifadhidata nyingi za serikali.
Kipf alikiri kwamba alifanya hivyo ili kuepuka majukumu yake ya malezi ya mtoto ya zaidi ya $100,000.
Mdukuzi huyo pia alipata mifumo mingine ya usajili wa vifo na makampuni katika uvamizi usiohusiana na tukio hilo ambao alitekeleza kwa kutumia nambari za siri zilizoibwa katika maelezo ya madaktari na wafanyakazi.
Aligunduliwa kuwa amejitolea kuwezesha wengine kufikia mifumo hiyo kwa malipo na kuuza hifadhidata zilizoibiwa zenye taarifa za kibinafsi kama Nambari za Usalama wa Jamii kwa wahalifu wengine wa mtandaoni.