Starlink ya Elon Musk yapigwa marufuku Brazil

Starlink, kampuni ya Musk ya kutoa huduma za ufikiaji wa intaneti ilikuwa imejikusanyia takribani watumiaji 250k nchini Brazil.

Muhtasari

• Mapema wiki hii, de Moraes alitishia kusimamisha mtandao wa kijamii wa X kote nchini ikiwa Musk hatatii maagizo yake.

• Katika majibu kwa watu walioshiriki ripoti za kufungiwa kwa Starlink nchini Brazil, Musk alimwita de Moraes "mhalifu wa aina yake mbaya kabisa, anayejifanya jaji".

Image: BBC

Akaunti za benki za Starlink ya SpaceX zimezuiwa nchini Brazili huku kukiwa na mzozo kati ya Jaji wa Mahakama ya Juu na Mkurugenzi Mtendaji wa X Elon Musk kuhusu kuzuia akaunti za mrengo wa kulia kwenye jukwaa la X.

Starlink inasema akaunti zao zimesitishwa nchini Brazil huku kukiwa na mzozo kati ya Alexandre de Moraes, jaji wa Mahakama ya Juu ya Brazil na bilionea wa teknolojia Elon Musk kuhusu jukwaa lake la mtandao wa kijamii X.

"Agizo hili linatokana na uamuzi usio na msingi kwamba Starlink inapaswa kuwajibika kwa faini inayotozwa - kinyume na katiba - dhidi ya X," Starlink inayomilikiwa na SpaceX iliandika katika taarifa kwenye jukwaa la X.

"Ilitolewa kwa siri na bila kuipatia Starlink mchakato wowote wa kisheria unaohakikishwa na Katiba ya Brazili. Tunakusudia kushughulikia suala hilo kisheria".

Katika majibu kwa watu walioshiriki ripoti za kufungiwa kwa Starlink nchini Brazil, Musk alimwita de Moraes "mhalifu wa aina yake mbaya kabisa, anayejifanya jaji".

Mapema wiki hii, de Moraes alitishia kusimamisha mtandao wa kijamii wa X kote nchini ikiwa Musk hatatii maagizo yake.

Kwa mujibu wa jarida la Euro News, Brazil ni soko muhimu kwa X na Starlink. Takriban Wabrazili milioni 40, au moja juu ya tano ya watu, hutumia ufikiaji wa X angalau mara moja kwa mwezi, kulingana na kikundi cha utafiti wa soko cha Emarketer na Starlink ina wateja takriban 250,000 nchini.

Haya yanajiri wakati ambapo kampuni za mawasiliano nchini Kenya zikilalama kuhusu Starlink ambayo wanahisi imekuja kuvuruga soko la huduma za ufikiaji intaneti nchini.