Mwanamume ashtumiwa kwa kuajiri watu asiowajua kumbaka mkewe

Polisi waligundua ubakaji 92 uliofanywa na wanaume 72.

Muhtasari

•Dominique anashtakiwa kwa kusajili watu asiowajua mtandaoni kuja nyumbani kwake na kumnyanyasa kingono mwathiriwa kwa zaidi ya muongo mmoja.

•Kesi hiyo imeitia hofu Ufaransa kwa ukubwa wa uhalifu huo wa kutisha .

Mhasiriwa wa dhuluma za kijinsia
GBV: Mhasiriwa wa dhuluma za kijinsia
Image: THE STAR

Mwanamume mmoja amefikishwa mahakamani nchini Ufaransa kwa kumpa mke wake dawa za kumlevya na kumbaka mara kwa mara na pia kupanga wanaume wengine kadhaa kumbaka.

Mshtakiwa huyo, aliyetajwa kwa jina la Dominique P, mwenye umri wa miaka 71, anashtakiwa kwa kusajili watu asiowajua mtandaoni kuja nyumbani kwake na kumnyanyasa kingono mwathiriwa kwa zaidi ya muongo mmoja.

Mwanamke huyo alikuwa ametulia sana hata hakujua kuhusu unyanyasaji huo uliorudiwa, mawakili wake wanasema.

Kesi hiyo imeitia hofu Ufaransa kwa ukubwa wa uhalifu huo wa kutisha .

Polisi waligundua ubakaji 92 uliofanywa na wanaume 72. Hamsini walitambuliwa na kushtakiwa na wapo mahakamani pamoja na mume wa mwathiriwa.

Mwathiriwa, ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 72, alifahamu kuhusu unyanyasaji huo mwaka wa 2020 baada ya kufahamishwa na polisi.

Kesi hiyo itakuwa "jambo la kutisha" kwake, alisema wakili wake Antoine Camus, kwani itakuwa mara ya kwanza kuona ushahidi wa video wa unyanyasaji huo.

"Kwa mara ya kwanza, atalazimika kuishi kupitia ubakaji ambao alivumilia zaidi ya miaka 10," aliambia shirika la habari la AFP.

Dominique P alichunguzwa na polisi baada ya tukio la Septemba 2020, wakati mlinzi alipomkamata akipiga picha kwa siri chini ya sketi za wanawake watatu katika kituo cha maduka.

Polisi kisha walipata mamia ya picha na video za mke wake kwenye kompyuta yake ambapo alionekana kupoteza fahamu.

Picha hizo zinadaiwa kuonyesha makumi ya mashambulizi katika nyumba ya wanandoa hao. Unyanyasaji huo unadaiwa kuanza mnamo 2011.