Tanzania yathibitisha kupungua kwa barafu ya Mlima Kilimanjaro

Kupungua kwa barafu kunaweza kuathiri mifumo ya hali ya hewa ya ndani.

Muhtasari

•Maeneo ya mito ya barafu ambayo wakati mmoja yalikuwa yakipanuka yamepungua kutoka kilomita za mraba 20 miaka 110 iliyopita hadi kilomita za mraba 1.7 tu hivi sasa.

Image: BBC

Afisa Mkuu wa Uhifadhi kutoka Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Mapinduzi Mdesa,amefichua kupungua kwa barafu ya Mlima Kilimanjaro, katika mahojiano na gazeti la The Citizen nchini Tanzania.

Maeneo ya mito ya barafu ambayo wakati mmoja yalikuwa yakipanuka yamepungua kutoka kilomita za mraba 20 miaka 110 iliyopita hadi kilomita za mraba 1.7 tu hivi sasa.

"Hii ni kwa sababu ya upepo mkali unaotoka baharini na maeneo mengine yanayofagia barafu. Kwa hiyo ni lazima tufanye juhudi za kuifanya Tanzania kuwa ya kijani," alisema katika mazungumzo na gazeti la The Citizen nchini Tanzania.

Kupungua kwa barafu ya Kilimanjaro, inayojulikana kwa mito yake ya barafu ya ajabu na kilele cha theluji, inaashiria athari kali za mabadiliko ya hali ya hewa kwenye moja ya alama za Afrika zinazotambulika zaidi.

Kupunguka kwa barafu sio tu dalili ya ongezeko la joto duniani lakini pia kunadhihirisha kupunguka kwa bioanuwaina raslimali yam aji katika eneo hilo

Tangazo la Mdesa lilileta mwanga wa haja ya haraka ya hatua za mazingira na kuonyesha changamoto zinazoendelea zinazowakabili wahifadhi na wanasayansi wanaofanya kazi ya kuhifadhi urithi wa kipekee wa asili wa Kilimanjaro.

Kupungua kwa barafu kunaweza kuathiri mifumo ya hali ya hewa ya ndani, bioanuwai, na usambazaji wa maji kwa jamii zinazozunguka.

Umoja wa Mataifa unasemaje?

Umoja wa Mataifa umetoa ripoti inayosema kuwa barafu duniani kote, ikiwa ni ile ya kwenye Mlima Kilimanjaro, zinatarajiwa kupotea ifikapo mwaka 2050 kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Hii ni pamoja na theruji katika maeneo ya Urithi wa Dunia ya Umoja wa Mataifa, kama vile Alps, na Hifadhi ya Taifa ya Yosemite nchini Marekani.

Licha ya juhudi za kimataifa za kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa, theruji hizi zitayeyuka bila shaka, kulingana na ripoti hiyo.

Kulingana na data za satelaiti, ripoti hiyo inaonyesha kuwa karibu mito ya barafu 18,600 katika maeneo 50 ya Urithi wa Dunia ya Umoja wa Mataifa, ambayo inawakilisha karibu 10% ya eneo la barafu la Dunia, ziko hatarini.

Maeneo haya sio tu maarufu ya utalii lakini pia yana umuhimu kwa jamii za mitaa.