Upinzani Tanzania watangaza maandamano kushinikiza kupatikana kwa waliotekwa

Mbowe ametoa rai kwa viongozi wote wa chama chake katika mikoa yote kujipanga na kupanga safari za kwenda Dar es salaam.

Muhtasari

•Chadema kimetangaza kufanya maandamano Septemba 23 katika jiji kuu la kibiashara, Dar es Salaam kuishinikiza Serikali kueleza walipo wanachama wao waliodaiwa kupotea.

Image: MAKTABA

Chama kikuu cha upinzani Tanzania, Chadema kimetangaza kufanya maandamano Septemba 23 katika jiji kuu la kibiashara, Dar es Salaam kuishinikiza Serikali kueleza walipo wanachama wao waliodaiwa kupotea.

Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe amesema, “Nimetangaza hadi kufikia September 21,2024 tunategemea tuone hatua za Watu kuwajibika kama hawatochukuliana hatua wenyewe kwa wenyewe sisi kuanzia September 23,2024 Jiji lote la Dar es salaam tutaandamana…

“… kila kata kila mtaa, mpo tayari?, Ndugu zangu tumekuwa tunafanya utani mara nyingi ‘this time around’ hatuna utani, kuanzia Jumatatu September 23,2024 sisi tutaingia barabarani kudai uhai wa watu wetu waliopotezwa labda Serikali ichukue hatua za haraka na za makusudi kuwarejesha, watu kujiuzulu na watu wote kuwajibika,” alisema Mbowe.

Mwanasiasa huyo mkongwe sambamba alitoa rai kwa viongozi wote wa chama chake katika mikoa yote kujipanga na kupanga safari za kwenda Dar es salaam kwaaajili ya maandamano hayo.

Alisema, “ wa Morogoro, Kanda ya Kati, Kusini, Kanda ya Nyasa, Magharibi, Victoria, Serengeti Kata ya Unguja na Pemba tutakutana Dar es salaam.”

Hatua hii inakuja siku chache baada ya kuuwawa kwa mjumbe wa sekretarieti ya chama hicho, Mohamed Ali Kibao ambaye alipotea na baadaye mwili wake kukutwa kwenye eneo la Ununio jijini Dar es Salaam.

UCHUNGUZI MAUAJI, UTEKAJI NCHINI TANZANIA

Mwanzo ni mwa juma, Rais wa Tanzania, Samia Suluhu aliagiza kupewa taarifa ya mauaji ya bwana Kibao na matukio mengine nchini.

Hata hivyo taarifa ya baadaye ya polisi waeleza kuwa wanaendelea kuchunguza matukio mbalimbali likiwemo hilo la Kibao

Jana Mwenyekiti wa Chadema alinukuliwa akisema kuwa polisi ndio washukiwa wakubwa wa mauaji na kwamba nchini Tanzania hakutakuwa na chunguzi huru iwapo wao ndio watakaochunguza.

Mbowe pia alisema, kisheria tume ya kijaji inayoundwa na Rais pia inaweza kuchunguza matukio hayo isipokuwa haitakuwa huru kwani inateuliwa na rais mwenyewe, hivyo wanataka vyombo vya uchunguzi kutoka nje ya Tanzania.

“Tumekubaliana watu pekee ambao tuna imani wanaweza kuja kufanya uchunguzi wa haki katika nchi yetu iwe lazima ni chombo cha kimataifa cha uchunguzi, na kipekee tumependekeza chombo kinachoitwa Scotland Yard kutoka Jeshi la Polisi la Uingereza kuja kufanya uchunguzi huu,” alisema Mbowe.