Zaidi ya wafungwa 250 watoroka jela baada ya mafuriko kubomoa ukuta

Mvua kubwa iliyonyesha kaskazini mashariki mwa Nigeria na kusababisha maafa zaidi

Muhtasari

• Wafungwa takribani mia tatu walifanikiwa kuhepa gerezani baada ya mafuriko ya mvua nyingi kunyesha kusababisha ukuta wa gereza kubomoka.

• Baadhi ya wafungwa waliotoroka walikuwa wanachama wa Boko Haram wa nchini Nigeria.

Kuporomoka kwa ukuta
Kuporomoka kwa ukuta
Image: Africa News//X

Zaidi ya wafungwa 250 wametoroka gerezani katika jiji la Maiduguru kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Wafungwa hao walifanikiwa kutoroka baada ya ua na ukuta wa gereza walimokuwa wamezuiliwa kubomoka kutokana na mafuriko ya mvua nyingi iliyoshesha sehemu hiyo kuanzia Jumanne ya tarehe 10.

Sehemu nyingi ya jiji la Maiduguri ilijaa maji baada ya bwawa la Alau kufurika na kingo zake kupasuka.

Mamlaka nchini Nigeria zimearifu kuwa angalau watu 30 waliangamia mamlaka hiyo ikikadiria kuwa huenda idadi hiyo ikaongezeka hata zaidi.

Aidha mamlaka hiyo imearifu kuwa watu milioni moja wameathirika na mafuriko hayo, yakiwawacha watu laki mbili bila makao.

Shirika la afya duniani WHO limeanza kutoa usaidizi wa dharura wa afya  kwa mamlaka ya Nigeria. Tayari WHO imewapeleka wahudumu 20 wa afya pamoja na dawa na bidhaa nyingine muhimu za afya katika maeneo yaliyoathirika mno Maiduguri

Inahofiwa kuwa baadhi ya wafungwa waliototoka ni wanachama wa mgambo wa Kiislamu wa Boko Haram.

Jiji la Maiduguri ndilo makao makuu ya jimbo la Borno sehemu ambayo wanamgambo wa Boko Haram wamekuwa wakitelekeaza uvamizi kwa wananchi sawia na jeshi kuanzia mwaka wa 2009.