Rwanda yawa nchi ya kwanza Afrika kutoa chanjo ya Mpox

Nchi hiyo jirani ilithibitisha wagonjwa wawili wa kwanza wa Mpox lakini hakuna aliyeripotiwa kufariki.

Muhtasari

•Rwanda imekuwa nchi ya kwanza barani Afrika kuanza kutoa chanjo hiyo mwezi wa saba mwaka huu.

Image: BBC

Wizara ya Afya ya Rwanda imetangaza kuwa imeanza kutoa chanjo dhidi ya ugonjwa wa homa ya Nyani (Mpox).

Kama ilivyotangazwa na afisa mkuu kutoka kituo cha Afrika cha kudhibiti magonjwa, Rwanda imekuwa nchi ya kwanza barani Afrika kuanza kutoa chanjo hiyo mwezi wa saba mwaka huu.

Rwanda ilithibitisha wagonjwa wawili wa kwanza wa Mpox lakini hakuna aliyeripotiwa kufariki dunia hadi hivi sasa.

Kulingana na Daktari Nicaise Ndembi kutoka Kituo cha Afrika cha Kudhibiti Magonjwa, Rwanda imekuwa nchi ya kwanzakutoa chanjo dhidi ya homa ya nyani – ambapo kwa mjibu wa wizara ya afya ya Rwanda zoezi la kutoa chanjo hiyo ni kuanzia, "wafanyabiashara wa mipakani, wahudumu wa afya, wafanyakazi wa hoteli na wengine walioko katika hatari ya kuambukizwa kwa urahisi".

Chanjo ambayo Rwanda ilianza kutoa ni dozi 1,000 ilizopewa na Nigeria miongoni mwa dozi 10,000 ambazo Marekani ilitoa kwa Nigeria mwishoni mwa mwezi uliopita wa Agosti, kulingana na maafisa wa Kituo cha Afrika cha Kudhibiti Magonjwa.

Mmoja wa wafanyakazi wa Wizara ya Afya nchini Rwanda aliambia BBC kwamba chanjo hii inatolewa kwa njia ya "Mobile Clinics" (magari yanayotoa huduma ya matibabu na yenye mahitaji yote) na kwamba zoezi hilo linatarajiwa kukamilika leo.

Jean Kaseya, mkuu wa kituo cha Afrika cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (Africa CDC), aliwaambia waandishi wa habari kwamba chanjo nchini Jamhuri ya demokrasi ya Kongo - ambayo inachukuliwa kuwa kitovu cha Mpox – itaanza kutolewa "wiki ya kwanza ya mwezi ujao".

Chanzo cha picha,Reuters

Kituo hicho kinasema kuwa chanjo nchini Rwanda ilianza Jumanne ya wiki hii ikilenga maeneo yanayopakana na DR Congo.

Mwezi Julai Rwanda ilithibitisha wagonjwa wawili wa kwanza wa Mpox. Wizara ya afya ilitangaza kwamba waliougua wamepona na hakuna aliyeripotiwa kuuawa hadi sasa.

Tangu mapema mwaka huu, Afrika imeripoti kesi 29,152 za Mpox na vifo 738 katika nchi 15.