Afisa mmoja mkuu wa umoja wa mataifa nchini Sudan amesema kwamba ametiwa wasiwasi mkubwa na ripoti za madhila makubwa ya kihalifu yanayotekelezwa katika jimbo la kati nchini Sudan la Gezira, ikiwemo mauaji ya halaiki ya raia yanayotekelezwa na kikosi maalum cha wanamgambo cha Rapid Support Force RSF.
Clementine Nkweta-Salami ametoa matamshi yake baada ya kundi la wanaharakati kusema kwamba watu 124 wameuawa na kikosi cha RSF kwenye mashambulizi yaliyotekelezwa kwenye vijiji katika wiki moja iliyopita.
RSF imekanusha shutuma hizo kwamba inawalenga raia, ikisema kwamba wapiganaji wake wanakabiliana na waasi waliopewa silaha na jeshi la Sudan.
Mzozo huo ambao umeendelea kwa miezi 18 sasa umesababisha vifo vya maelfu ya watu na kuwalazimisha wengine milioni 11 kuhama makwao.
Nkweta-Salam , ambaye ni msimamizi wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa mataifa nchini Sudan, amesema kwamba taarifa za awali zimeashiria kwamba RSF ilitekeleza mashambulizi mawili katika maeneo tofauti kwenye jimbo la Gezira kati ya Oktoba 20 na 25, 2024.
Aidha amesema kwamba hali hiyo ilichangia maafa ya watu wengi na kuwa shambulizi la halaiki, huku wanawake wakibakwa, nazo biashara zikiporwa na wengine kupora mali ya watu kwenye makazi ya kibinafsi na hata kuchoma mashamba ya watu.
Bi Nkweta - Salam amesema kwamba maovu hayo ya kihalifu ni saw ana kilichoshuhudiwa katika jimbo la Darfur mwaka wa 2023, wakati ambapo RSF ilishutumiwa kwa kutekeleza mauaji ya kimbari dhidi ya jamii ambazo zilionekana kupinga kikosi hicho.
Nkweta Salam, aidha amesema kwamba idadi kamili ya waliofariki haijulikani, lakini taarifa za awali zimeonyesha kwamba wengi waliuawa katika jimbo la Gezira.