Takribani watu 23 wameuawa katika mashambulizi ya anga ya Israel dhidi ya nyumba mbili katikati mwa Lebanon ambako familia zilizopoteza makazi ziliripotiwa kuishi, wizara ya afya ya Lebanon inasema.
Watu 15, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, waliuawa huko Joun na wengine wanane waliuawa karibu na Baalchmay. Vijiji vyote viwili viko katika eneo la Mlima Lebanon na maeneo ya nje ambako kundi lenye silaha la Hezbollah lina uwepo mkubwa.
Jeshi la Israel lilisema lilikuwa likichunguza mashambulizi hayo, ambayo yalikuja baada ya kugonga kile ilichosema ni malengo kadhaa ya Hezbollah katika vitongoji vya kusini mwa Beirut.
Wakati huohuo, watu wawili waliuawa kutokana na kurushwa kwa roketi ya Hezbollah katika mji wa Nahariya kaskazini mwa Israel.
Ilikuja siku moja baada ya waziri wa ulinzi wa Israel kukataa kusitisha mapigano na Hezbollah hadi malengo yake ya vita yatimizwe.
Jeshi la Israel lilifanya mashambulizi dhidi ya Hezbollah, ambayo inaidhinisha kama shirika la kigaidi, baada ya karibu mwaka wa mapigano ya kuvuka mpaka yaliyosababishwa na vita huko Gaza.
Israel inasema inataka kuhakikisha wanarejesha salama makumi ya maelfu ya wakaazi wa eneo la mpaka wa kaskazini mwa Israel waliokimbia makazi yao kutokana na mashambulizi ya roketi, ambayo Hezbollah ilianzisha kuunga mkono Wapalestina siku moja baada ya shambulio baya la mshirika wake Hamas dhidi ya Israel tarehe 7 Oktoba 2023.
Zaidi ya watu 3,200 wameuawa nchini Lebanon tangu wakati huo, ikiwa ni pamoja na 2,600 katika wiki saba tangu Israel ianzishe kampeni kali ya anga na kufuatiwa na uvamizi wa ardhini kusini, kulingana na wizara ya afya ya Lebanon. Watu wengine milioni 1.2 wamelazimika kuyahama makazi yao.