Raia wawili wa Uganda wamekamatwa kwa tuhuma za kuwatusi Rais Yoweri Museveni, mkewe Janet Museveni na mtoto wa Rais, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, kwenye mtandao wa kijamii wa TikTok.
Jaji Stella Maris Amabilis aliamuru kuwa David Ssengozi, mwanzilishi wa Lucky Choice, mwenye umri wa miaka 21, na Isaya Ssekagiri mwenye umri wa miaka 28, warudishwe rumande katika gereza la Kigo hadi Jumatano, ambapo wanatarajiwa kufikishwa mahakamani.
Wanadaiwa kutumia matamshi ya chuki na kueneza habari mbaya kuhusu familia ya rais na wanamuziki wanaohusishwa na chama tawala cha NMR.
Walipofika mahakamani Jumatatu, wawili hao walikanusha mashtaka dhidi yao.
Wanashtakiwa pamoja na Julius Tayebwa, 19, ambaye tayari amefikishwa mahakamani alikini akiwa bado yuko gerezani kwa makosa sawa na hayo. Waendesha mashtaka wanasema kwamba waliochapisha habari hizo kwenye TikTok wanalenga "kukashifu, kudharaulisha, na kueneza chuki" dhidi ya familia ya Rais Museveni na watu wengine.
Hakimu aliidhinisha kuzuiliwa kwao baada ya polisi kusema kuwa bado wanachunguzwa.
Septemba 9 mwaka huu, msemaji wa jeshi la polisi nchini Uganda, Rusoke Kituuma alionya kuwa kumtukana rais aliyemtaja kuwa ni chanzo cha heshima ni kosa.
Haijabainika ni ujumbe gani uliosababisha kukamatwa kwake, lakini katika video iliyochapishwa kwenye TikTok tarehe 4 Aprili mwaka huu kwenye ukurasa wa LuckyChoice70, wenye kichwa "maadui wangu wa kwanza", aliikosoa familia ya rais kwa kutumia lugha chafu zinazohusiana na ngono.