Mke wa kiongozi wa upinzani nchini Uganda Kizza Besigye anasema mume wake ametekwa nyara na sasa anazuiliwa katika jela ya kijeshi.
Katika taarifa kwenye X, Winnie Byanyima aliandika kwamba mumewe alikamatwa katika mji mkuu wa Kenya Nairobi siku ya Jumamosi iliyopita wakati wa hafla ya uzinduzi wa kitabu.
"Nimefahamishwa kuwa yuko katika jela ya kijeshi huko Kampala," aliandika, na kuitaka serikali ya Uganda kumwachilia mumewe.
BBC News imewasiliana na serikali ya Uganda kutoa maoni yake kuhusu suala hilo.
Besigye, 68, aliongoza chama cha siasa cha Forum for Democratic Change (FDC), akigombea na kushindwa katika chaguzi nne za urais dhidi ya Yoweri Museveni, ambaye yuko madarakani tangu 1986.
"Sisi familia yake na wanasheria wake tunataka kumuona," mkewe aliandika kwenye X.
"Yeye si mwanajeshi. Kwa nini anazuiliwa kwenye jela ya kijeshi?"
Winnie Byanyima ni mtetezi wa haki za binadamu na mkurugenzi mtendaji wa Unaids, mpango wa pamoja wa Umoja wa Mataifa ambao ulianzishwa ili kutokomeza Ukimwi.
Kizza Besigye aliwahi kuwa daktari wa binafsi wa Museveni lakini aliamua kuwa kiongozi wa upinzani na amemtaja kiongozi wa nchi hiyo ya Afrika Mashariki kama "dikteta."
Amedai kuwa chaguzi zilizopita za urais ziliibiwa - madai ambayo yamekanushwa na serikali.
Kiongozi huyo wa upinzani amekamatwa mara kadhaa huko nyuma.
Wakati mmoja alipigwa risasi mkononi, na pia aliwahi pata jeraha la jicho baada ya kumwagiwa maji ya kuwasha.
Serikali inashutumu kwa uchochezi, na amewahi kufunguliwa mashtaka ya kuchochea vurugu.