Takribani watu 24 wamefariki baada ya boti mbili zilizokuwa zimewabeba raia wengi wa Somalia kupinduka katika pwani ya Madagascar, mamlaka za eneo zilisema.
Taarifa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Somalia ilisema juhudi zinaendelea "kuhakikisha kuwa manusura wanarejea salama".
Boti hizo mbili zilibeba jumla ya abiria 70.
Ziligunduliwa zikiwa ziko karibu na pwani ya kaskazini mwa Madagascar siku ya Jumamosi katika Bahari ya Hindi.
Inaaminika injini zao zilifeli. Afisa mkuu wa serikali ya Somalia aliviambia vyombo vya habari vya ndani kuwa manusura waliokolewa na wavuvi.
Walionusurika wanasema walikuwa wakijaribu kufikia kisiwa cha Ufaransa cha Mayotte, njia ya kawaida lakini hatari kwa wahamiaji wa Kisomali wanaotafuta hifadhi.
Ukosefu wa ajira na umaskini katika Pembe ya Afrika unawalazimu vijana wengi kuchukua njia hatari ya kufika Ulaya kwa matumaini ya maisha bora.
Mamlaka ya Madagascar ilionya dhidi ya "hatari kali zinazohusiana na uhamiaji haramu" ikipendekeza waathiriwa wa janga hilo walikuwa wahamiaji.