Mwenyekiti wa zamani wa Benki ya Uchina, Liu Liange, mnamo Jumanne alihukumiwa kifo baada ya mahakama moja mjini Jinam katika mkoa wa Shandong mashariki mwa China kumpata na hatia ya kupokea rushwa na utoaji wa mikopo kinyume cha sheria.
Mahakama hiyo ilibaini kuwa Liange alipokea hongo yenye thamani ya zaidi ya Yuan milioni 121 sarafu ya Uchina ikiwa ni sawia na dola milioni 16.8 za Marekani.
Katika uamuzi uliotolewa na korti hiyo, kwa mujibu wa shirika moja la habari la serikali nchini humo, Liu Liange alinyimwa haki za kisiasa za maisha yake yote baada ya kupatikana na hatia. Vile vile, mali yake yote ya kibinafsi itachukuliwa na faida zake zote alizopata kwa njia za haramu zitarejeshwa na kukabidhiwa hazina ya serikali.
Mahakama iligundua kuwa Liu akitumikia benki za Export-Import ya China na Benki ya China katika nafasi mbali mbali za uongozi alitumia fursa hizo kupokea hongo kinyume cha sheria ili kusaidia wengine katika masuala kama vile ufadhili wa mikopo, ushirikiano wa miradi na mipango ya wafanyakazi.
Liu
Liange aidha, alipatikana na hatia ya kuwezesha utoaji wa mikopo ya jumla ya zaidi
ya Yuan bilioni 3.32 kwa makampuni yasiyo na sifa kinyume na sheria za kisheria
licha ya kuwa na ufahamu pamoja na kusababisha hasara kuu ya zaidi ya Yuan
milioni 190.7 sawa na dola milioni 27.