BENKI ya Uganda imetumbukia katika kashfa mpya baada
ya wadukuzi kujipatia shilingi bilioni 2.2 (takriban dola milioni 17 za
Kimarekani) kutoka kwa mifumo ya benki hiyo, jarida la The Citizen limeripoti.
Tukio hilo la udukuzi, ambalo linaaminika kutokea
hivi karibuni, limezua maswali mazito kuhusu hatua za kiusalama zinazochukuliwa
katika benki kuu.
"Ni
kweli, Rais Museveni alimwagiza Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuchunguza
suala hilo," chanzo kilicho karibu na suala hilo kiliiambia
CNN.
"Mkaguzi
Mkuu wa Hesabu za Serikali atabaini kiasi cha fedha kilichopotea katika udukuzi
huo na kisha polisi watafuatilia pale ambapo kuna dhima ya uhalifu."
Benki ya Uganda bado haijatoa maoni yoyote kuhusu
wizi huo, lakini duru zinasema uchunguzi uko katika hali ya juu, huku maafisa
wa ngazi za juu wakihojiwa na polisi na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.
Benki kuu imekabiliwa na kashfa katika miaka ya hivi
karibuni, ikiwa ni pamoja na wizi wa noti za zamani na maafisa wake.
Katika kesi mashuhuri, Charles Kasede Ochieng,
aliyekuwa Mkuu wa Uhakiki, alihukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela kwa
kutumia vibaya nafasi yake kuiba noti kuukuu zilizokusudiwa kuharibiwa.
Kashfa ya hivi punde imeibua wasiwasi kuhusu uwezo wa
benki hiyo kulinda mifumo yake na athari zinazoweza kujitokeza kwa uchumi wa
nchi.
Benki ya Uganda imekuwa bila gavana tangu kifo cha
Emmanuel Mutebile Januari 2022.
Hii si mara ya kwanza kwa tukio la udukuzi kufanyika katika
mifumo ya Benki kuu ya Uganda.
Mnamo Agosti 2020, ripoti ziliibuka kwamba wadukuzi walifanya
jaribio la kutaka kuiba dola milioni 24 baada ya kudukua mitambo ya benki hiyo.
Kwa mujibu wa ripoti wakati huo, akaunti ambazo zililengwa
ni zile za idara zenye mgao mkubwa wa bajeti kama wizara ya ulinzi, kawi, ujenzi
wa miundombinu na kilimo.
Hata hivyo, baadhi ya pesa ambazo zilikuwa tayari
zimehasmishiwa kwa akaunti zilizokuwa Hong Kong na UAE zilifaulu kurudishwa.
Tayari, rais Museveni ametoa agizo la kufanyika kwa
uchunguzi dhidi ya udukuzi huo ambao umeonekana kuwa donda sugu kwa usalama wa
mifumo ya benki ya Uganda.