logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Gaza inazidi kukumbwa na janga ya kibinadamu ambalo UNFPA inasema halijawahi kutokea.

Watu zaidi ya 45,000 wameuliwa kwenye mzozo huo, asilimia 70 ya vifo hivyo ikiwa ni watoto

image
na Brandon Asiema

Kimataifa16 December 2024 - 12:14

Muhtasari


  • UN inahofia kwamba takribani wanawake 50,000 ambao ni wajawazito watakumbwa na wakati mgumu haswa majira ya baridi yanapokaribia.
  • Licha ya changamoto hizo, UNFPA imesema kwamba imewafikia watu 98,000 ndani ya mwezi Novemba, watu Zaidi ya 25,000 wakisaidika na huduma za kuokoa maisha.


Taarifa ya mfuko wa Umoja wa Mataifa wa idadi ya watu UNFPA kuhusu hali ya ubinadamu katika ukanda wa Gaza inaashiria kuwa janga la kibinadamu linaloshuhudiwa katika eneo hilo halijawahi kutokea ikikadiriwa idadi ya vifo na maafa ambayo yameshuhudiwa tangu kuanza kwa vita baina ya jeshi la Israel na wanamgambo wa Hamas mnamo Oktoba mwaka 2023.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyotolewa Disemba 12, Gaza inakabiliwa na janga la kibinadamu ambalo halijawahi kutokea, watu zaidi ya 45,000 wakiwa wameuawa asilimia kubwa ikiwa ya watoto. Watoto waliouliwa kufuatia mzozo huo ni takribani asilimia 70 na vifo hivo.

Vile vile, kwenye taarifa hiyo watu wapatao 110,000 wamepatwa na majeraha mbali mbali huku idadi ya watu milioni 1.9 wakiwa wamefurushwa makao yao mara kwa mara kutokana na mashambulizi baina ya vikosi viwili vinavyozozana.

UN imeripoti kwamba miundo misingi ya Gaza imeharibiwa vibaya ikihusiisha hospitali na miundo mbinu ya maji na usafi. Katika maeneo ya Gaza, ni hospitali 17 pekee kati ya 36 zinazohudumu ila UN imetahadhari kwamba huduma kutoka kwa vituo hivyo vya afya 17, ni ya chini mno, hospitali nyingi zikikosa usambazaji wa kutosha wa bidhaa za matibabu na chakula.

UN inahofia kwamba takribani wanawake 50,000 ambao ni wajawazito watakumbwa na wakati mgumu haswa majira ya baridi yanapokaribia.

“Wanawake na wasichana huko Gaza, wakiwemo wajawazito 50,000 wameachwa bila mahitaji muhimu ya kuishi. Majira ya baridi kali yanapoanza, chakula hakitoshelezi, vifa vya kujikinga ni haba sana, maji, hali ya usafi inazidi kuzorota hata Zaidi na viwango vya kutisha vya ukosefu wa chakula na utapiamlo vinazidi kuwa mbaya zaidi”  Sehemu ya ripoti yake ilisema.



Hata hivyo licha ya ugumu unaoshuhudiwa na watu wanaoathirika na mzozo huo, UNFPA imesema  juhudi zake za kufikisha msaada kwa maeneo yaliyoathirika mno inakumbwa na vizingiti. UNFPA imedai kwamba vikwazo hivyo vimesababisha malori 49 ya msaada yaliyobeba vifaa vya afya ya uzazi vya kuwasaidia wanawake wajawazito yamezuiliwa mpakani yakisubiri kuingia Gaza.

Malori mengi, yamepiga kambi mpakani hapo tangu mwezi Septemba yakiwa na mahema, sodo, vifaa vya usafi na genereta za kusaidia katika uzalishaji wa umeme.

Licha ya changamoto hizo, UNFPA imesema kwamba imewafikia watu 98,000 ndani ya mwezi Novemba, watu Zaidi ya 25,000 wakisaidika na huduma za kuokoa maisha.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved