Watu saba huko Fiji walipelekwa hospitalini ikishukiwa wamekunywa sumu baada ya kunywa kileo cha matunda kwenye baa ya hoteli ya nyota tano, serikali ya eneo hilo imesema.
Watano ni watalii, huku mmoja akitoka Marekani na wengine kutoka Australia, wenye umri wa kati ya miaka 18 na 56. Wengine wawili ni wageni wanaoishi Fiji, kulingana na ripoti za vyombo vya habari nchini humo vikinukuu wizara ya afya.
Tukio hilo linakuja wiki kadhaa baada ya vifo vya watalii sita katika taifa la Kusini Mashariki mwa Asia la Laos kwa sababu ya sumu ya methanoli.
Mkuu wa utalii wa Fiji, Brent Hill aliiambia RNZ kuwa wanafahamu vyema tukio la Laos, lakini kesi ya Fiji ni "mbali na tukio hilo."
Muda mfupi baada ya kunywa pombe katika hoteli ya Warwick Fiji kwenye Pwani ya Coral, wageni saba walipata kichefuchefu, kutapika na shida katika mifumo ya hisia.
Awali walipelekwa katika Hospitali ya Sigatoka, na baadaye kuhamishiwa Hospitali ya Lautoka, kwa mujibu wa gazeti la Fiji Times.
Uchunguzi wa awali unaendelea na hakuna kesi zaidi zilizoripotiwa, mamlaka ilisema.