WATU wawili wamekamatwa kwa madai ya kupanga njama ya
kumdhuru Rais wa Zambia Hakainde Hichilema kwa kutumia uchawi, polisi walisema
Ijumaa.
Msemaji wa polisi, Rae Hamoonga alisema katika
taarifa yake kwamba washukiwa hao wawili, Jasten Mabulesse Candunde, 42, na
Leonard Phiri, 43, wanadaiwa kukodiwa na Nelson Banda, mdogo wa mbunge mtoro
Jay Banda, ili kumroga rais.
Jay Banda alitoroka kutoka mikononi mwa polisi Agosti
2024 akikabiliwa na shtaka la wizi wa kupindukia. Mahali alipo hajulikani.
Washukiwa hao wawili wanakabiliwa na mashtaka ya
kufanya uchawi, kumiliki hirizi na ukatili kwa wanyama.
"Washukiwa hao walikutwa na hirizi za aina
mbalimbali, akiwemo kinyonga aliye hai, na wanadaiwa kuwa waganga,"
Hammonga alisema, na kuongeza kuwa dhamira yao "ilikuwa ni kutumia hirizi
kumdhuru Mkuu wa Nchi, Mheshimiwa Rais Hakainde Hichilema.”
Msemaji wa polisi alisema washukiwa hao walifichua
kwamba walikubali kupokea malipo kamili ya $7,400.
"Dhamira yao iliyodaiwa ilikuwa kutumia hirizi
kudhuru" Rais Hakainde Hichilema, alisema taarifa ya polisi, iliyotolewa
Ijumaa.
Watu wengi katika nchi hiyo ya kusini mwa Afrika
wanaamini - na wanaishi kwa hofu ya - uchawi.
Polisi walisema Bw Candunde na Bw Phiri waliajiriwa
na Nelson Banda, nduguye mdogo wa Mbunge Emmanuel “Jay Jay” Banda.
Mbunge huyo aliripotiwa kukamatwa mwezi uliopita
katika nchi jirani ya Zimbabwe kutokana na mashtaka ya wizi, ambayo
anayakanusha, lakini hajaonekana hadharani.
Pia anadaiwa kutoroka kutoka kizuizini mwezi Agosti
alipokuwa akisubiri kufikishwa mahakamani.
Chama cha upinzani cha Patriotic Front (PF),
kinachoongozwa na Rais wa zamani Edgar Lungu, hapo awali kilidai kuwa mashtaka
haya yanachochewa kisiasa.
Emmanuel Banda, ambaye amekuwa mbunge huru tangu
2021, awali alihusishwa na Lungu, ambaye alipoteza urais na Hichilema mwaka
huo.
Katika taarifa yao, polisi walisema kwamba mdogo wa
mbunge huyo, Nelson, "kwa sasa yuko mbioni".
Bw Candunde na Bw Phiri wameshtakiwa chini ya Sheria
ya Uchawi ya Zambia kwa "kumiliki hirizi", "kudai ujuzi wa
uchawi" na "ukatili kwa wanyama pori".
Wawili hao walipatikana na "hirizi
mbalimbali", akiwemo kinyonga aliye hai, polisi waliongeza.
Washukiwa hao wanazuiliwa na watafikishwa mahakamani
"hivi karibuni", polisi walisema, lakini hawakutoa tarehe kamili ya
kusikilizwa kwa kesi hiyo. Bado hawajazungumza hadharani kuhusu tuhuma hizo.