Mtu mwenye silaha amewaua kwa risasi watu 12, wakiwemo watoto wawili, kusini mwa Montenegro, polisi wamesema.
Shambulio la Jumatano lilitokea ndani ya mkahawa katika eneo la Cetinje kufuatia mabishano ya maneno, kulingana na serikali.
Serikali ya nchi hiyo imetangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa kuanzia Alhamisi, huku Waziri Mkuu Milojko Spajic akisema ufyatuaji risasi "umechafua nchi yetu.”
Polisi walisema shambulio hilo lilianza pale mwanamume aliyeitwa Aleksandar Martinović, 45 - alipofyatua risasi katika mkahawa huo.
Aliwaua watu wa familia yake, watoto wawili wa mmiliki wa mgahawa huo - wenye umri wa miaka 10 na 13 - na pia mmiliki, kulingana na kamanda wa polisi wa Montenegro.
Mshambuliaji huyo kisha akaendelea kuua watu zaidi katika maeneo mengine.
Kulingana na polisi, mshukiwa alikuwa amekunywa pombe kupita kiasi kabla ya shambulio hilo kuanza.
Watu wanne walipelekwa hospitalini baada ya kujeruhiwa vibaya kwa risasi.
Mshambulizi huyo alikimbia lakini baadaye alijijeruhi vibaya baada ya kuzingirwa na polisi waliomtaka adondoshe silaha yake, polisi walisema.
Alifariki akiwa njiani kupelekwa hospitali.