Mamilioni ya Wamarekani wanatazamia majira ya baridi kali ambayo inaweza kusababisha kushuhudiwa kiwango kikubwa cha theluji katika kipindi cha muongo mmoja.
Baridi kali ilianza katikati mwa nchi, na itasonga mashariki katika siku chache zijazo, idara ya hali ya hewa nchini humo NWS inasema.
Hali ya hatari imetangazwa katika Majimbo ya Kentucky, Virginia, Kansas, Arkansas na Missouri.
Katikati mwa Marekani, kutakuwa na "mvurugiko mkubwa wa shughuli za kila siku" na "hali ya hatari au isiyoruhusu uendeshaji wa magari na hivyo kufungwa kwa kiasi kikubwa" hadi Jumapili, kwa mujibu wa mamlaka ya hali ya hewa NWS.
Mtangazaji wa BBC wa masuala ya hali ya hewa Elizabeth Rizzini anaonya kuhusu "hali mbaya ya kusafiri" siku nzima ya Jumapili huku theluji kubwa ikinyesha, haswa katika maeneo ya kaskazini yaliyokumbwa na dhoruba.
Jumla ya majimbo 30 yamewekwa chini ya tahadhari ya hali ya hewa huku dhoruba hiyo ikitarajiwa kusafiri kuelekea mashariki mwa nchi.
Zaidi ya safari 2,000 za ndege zimechelewa na 1,500 kughairishwa kuingia na kutoka Marekani leo, kwa mujibu wa tovuti inayofuatilia safari za anga.
Hali kama hiyo imeshuhudiwa pia nchini Uingereza ambako abiria wanakabiliwa na kuahirishwa na kucheleweshwa kwa safari baada ya viwanja vya ndege kadhaa nchini humo kulazimika kufunga njia zake za ndege huku theluji na mvua ikinyesha sehemu kadhaa za Uingereza.