Kampuni ya Marekani inayotoa hujduma za watumizi wa mtandao kuchakura maswala mbali mbali mtandaoni ya Google imechanga dola milioni moja sawia na shilingi milioni 129.45 za Kenya kwa ajili ya maandalizi ya hafla ya uapisho wa rais mteule wa Marekani Donald Trump.
Donald Trump alishinda uchaguzi wa Marekani wa mwaka jana kwa kumpiku naibu wa rais anayeoondoka Khamala Harris na anatarajiwa kuapishwa na kuanza kuiongoza Marekani rasmi Januari tarehe 20. Huu utakuwa muhula wa pili kwa Trump kuingia ikulu ya White House.
Mbali na kuchangia fedha hizo, kampuni ya Google vile vile imesema kwamba itapepereusha matukio ya siku ya uapisho wa Trump moja kwa moja duniani kwote.
Mkuu wa masuala ya serikali duniani na sera za umma Karan Bhatia amehakikisha kuwa upeperushaji huo utafanyika kwenye jukwaa la Youtube na ukurasa wa nyumbani wa mtandao wa Google.
“Google inafuraha kuunga mkono uapisho wa 2025, kwa kupeperusha hafla hiyo moja kwa moja kwenye Youtube na uunganisho wa moja kwa moja kwenye ukurasa wetu wa nyumbani.” Karan Bhatia alisema.
Aidha mbali na kampuni ya Google, kampuni ya anga inayounda, kutengeneza na kuhudumia ndege za kibiashara na kijeshi, pamoja na mifumo ya anga ya Boeng pia imechangia kiasi sawia cha hela kwa ajili ya hafla hiyo ya uapisho.
Vile vile kampuni nyingine za kimataifa za Marekani zimetoa michango yao kuelekea uapisho wa Trump wa Januari 20. Kampuni hizo ni ikiwemo kampuni za kutengeneza magari ya Toyota, Ford na General Motors.
Kampuni za Uber, Meta, Amazon na kampuni ya kuzalisha mafuta
ya Chevron pia zimetoa michango yao kwa kamati inayoandaa uapisho huo.