Chama tawala nchini Tanzania, Chama cha Mapinduzi (CCM) kimepitisha azimio la kumteua Rais Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea wa nafasi ya urais katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika baadae mwaka huu.
Azimio hilo limepitishwa na Mkutano Mkuu wa CCM ambao ndiyo chombo cha mwisho cha maamuzi ya uteuzi wa mgombea wa tiketi ya urais kupitia chama hicho. Chama hicho pia kimempitisha Dkt. Hussein Mwinyi kugombea Urais kwa upande wa Zanzibar.
Uamuzi huo umefanyika mapema kuliko kawaida, na katika mkutano ambao awali haukupangwa kufanya maamuzi hayo katika ajenda zake. Mkutano huo ulikuwa na ajenda kuu moja ya kupitisha jina la Makamu wa Mwenyekiti (Bara) ambapo mwanasiasa mkongwe Stephen Wasira alipitishwa kushika wadhifa huo jana Jumamosi.
Awamu ya mwisho kwa Samia na Mwinyi
Marais wote wawili Samia na Mwinyi wanamaliza awamu zao za kwanza za uongozi mwaka huu. Na kwa mujibu wa utamaduni wa chama hicho, marais walio madarakani huwa hawapatiwi ushindani katika kupewa tiketi ya kugombea urais kwa awamu ya pili.
Rais Samia aliingia madarakani mwezi Machi 2021 mara baada ya kifo cha aliyekuwa rais wa Tanzania John Pombe Magufuli. Aliingia madarakani kwa mujibu wa katiba akiwa ndiye mrithi wa urais, kwa nafasi aliyokuwa nayo kipindi hicho ya Makamu wa Rais.
Kwa mujibu wa katiba ya Tanzania, kwa kuwa amekaa madarakani kwa zaidi ya miaka mitatu toka kufariki kwa Magufuli basi kipindi hiki kinahesabika kama muhula wake kamili na ataruhusiwa kugombea urais mara moja tu.
"Endapo Makamu wa Rais anashika kiti cha Rais kwa mujibu wa masharti ya ibara ya 37(5) kwa kipindi kinachopungua miaka mitatu ataruhusiwa kugombea nafasi ya Rais mara mbili, lakini kama akishika kiti cha Rais kwa muda wa miaka mitatu au zaidi ataruhusiwa kugombea nafasi ya Rais mara moja tu," inaeleza katiba ya Tanzania.
Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue
Hivyo baada ya kupitishwa kuwa mgombea leo na endapo atashinda urais katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu, ukomo wa Rais Samia kushika Madaraka ya urais utakuwa nim waka 2030.
Hivyo hivyo itakuwa kwa upande wa Zanzibar kwa Rais Mwinyi ambaye aligombea kwa mara ya kwanza urais mwaka 2020, baada ya kupitia mchujo wa ushindani ndani ya chama.