Mke wa rais anayekuja, Melania Trump amezindua sarafu yake ya mtandaoni usiku wa kuamkia kuapishwa kwa mumewe kama rais wa Marekani.
Tangazo hilo linakuja saa chache baada ya Rais mteule Donald Trump naye kuzindua sarafu yake ya mtandaoni ya $Trump.
Alichapisha taarifa ya sarafu yake ya $MELANIA kwenye mtandao wa kijamii wa X siku ya Jumapili.
Kulingana na tovuti ya CoinMarketCap, $Trump ina thamani ya jumla ya dola za kimarekani bilioni 12, huku ya $Melania ikiwa na thamani ya dola 1.7.
Katika siku za nyuma Trump aliwahi kuiita sarafu ya mtandaoni kuwa ni utapeli, lakini wakati wa kampeni za uchaguzi wa 2024 alikuwa mgombea wa kwanza wa urais kukubali michango kupitia sarafu hizo za kidijitali.
Katika kampeni, Trump pia alisema ataunda hifadhi ya kimkakati ya sarafu ya bitcoin na kuteua wadhibiti wa fedha ambao wana mtazamo chanya kuhusu sarafu za mtandaoni.
Kufuatia ushindi wa Trump, sarafu ya bitcoin ilipanda thamani. Na kwa sasa bitcoin moja ni sawa na dola ya Marekani 107,000, kulingana na Coinbase.
Sarafu nyingine, ikiwa ni pamoja na dogecoin - ambayo imepigiwa upatu na mfuasi wa Trump, bwana Elon Musk - pia imeongezeka thamani mwaka huu.
Chini ya Rais Joe Biden, wasimamizi wa fedha walieleza wasiwasi wao kuhusu sarafu za mtandaoni wakija utapeli na utakatishaji wa pesa na wakakabiliana na kampuni za sarafu hizo za kidigitali.