
Maelfu ya waandamanaji wametokea mitaani Uturuki baada ya mpinzani mkuu wa Rais Recep Tayyip Erdogran kukamatwa na kushtakiwa kwa kosa la ufisadi.
Ekrem Imamoglu, meya wa Istanbul, alikuwa akitarajiwa kuteuliwa kama mgombea wa Urais wa chama cha Republican People's Party's (CHP) 2028 siku ya Jumapili.
Kufuatia kukamatwa kwake, maandamano yalishuhudiwa waandamanaji wakikabiliwa vikali na maafisa wa usalama kwa mabomu ya vitoa machozi na risasi za mpira ili kuwatawanya.
Imamoglu kwa upande wake anasema madai dhidi yake yamechochewa na siasa.
'' Sitatetereka,'' aliandika kupitia mtandao wake wa kijamii wa X kabla ya kuzuiliwa rumande.
Rais Erdrogan ameshutumu vikali maandamano na kulaumu chama cha CHP kwa kujaribu ''kutatiza amani na kugawanya watu''.
Waandamanaji walikusanyika karibu na makao ya jiji la Istanbul na kuonekeana wakipeperusha bendera za Uturuki huku wakiimba nyimbo mbele ya maafisa wa polisi wanaoshika doria.
Maafisa wa usalama walionekana wakiwarushia waandamanaji maji ya kuwasha ili kuwadhibiti.
Mkewe Imamoglu kwa jina Dilek Kaya alihutubia waandamanaji akiwaambia kuwa 'udhalimu' anaopitia mumewe na umevuka mipaka.
Zaidi ya watu 700 wamekamatwa tangu kuanza kwa maandamano hayo, kwa mujibu wa mamlaka ya Uturuki.
"Niko hapa kwa ajili ya haki, niko hapa kwa ajili ya uhuru. Sisi ni watu huru na watu wa Uturuki hawawezi kukubali hili. Hii ni kinyume na tabia na utamaduni wetu,'' mwandamaji mmoja anasema.
CHP ilikuwa na muungano wa kweli na Chama cha Usawa na Demokrasia cha Watu wa Kurdish (DEM) kuhusiana na uchaguzi wa mitaa wa mwaka jana. DEM imeshutumiwa kwa kuhusishwa na PKK - au Kurdistan Workers' Party - ambayo inakanusha.
Kundi la PKK lilitangaza kusitisha mapigano mapema mwezi huu, baada ya kuendesha uasi dhidi ya Uturuki kwa zaidi ya miaka 40. Imepigwa marufuku kama kundi la kigaidi nchini Uturuki, Umoja wa Ulaya, Uingereza na Marekani.
Maandamano ya kujibu kukamatwa kwa Imamoglu ni makubwa zaidi kuwahi kutokea nchini humo tangu maandamano ya Gezi ya mwaka 2013, yaliyoanza mjini Istanbul kuhusu kubomolewa kwa bustani ya eneo hilo.