Mkutano kati ya ujumbe wa Marekani na kundi la wapatanishi wa Urusi wa mpango wa kusitisha mapigano nchini Ukraine ulifanyika mjini Riyadhi.
Wamarekani walifanya mazungumzo na ujumbe wa Kyiv siku ya Jumapili. Kama ilivyotangazwa, wajumbe wote watatu hawakukusanyika kwenye meza moja.
Kulingana na ripoti za shirika la habari la Urusi, mazungumzo hayo yalidumu kwa takriban saa 12. Kulingana na vyanzo vya mashirika ya habari ya TASS na RIA Novosti. Taarifa ya pamoja kufuatia mazungumzo hayo inaweza kuwekwa wazi mnamo Machi 25, 2025.
Hakuna taarifa za mafanikio zilizotarajiwa kutoka kwa duru hii: Volodymyr Zelensky alizungumza kuhusu hali ya mazungumzo ya "kiufundi" ya mkutano huo, na Urusi ilituma maafisa wa ngazi za chini kwenda Saudi Arabia. Mazungumzo yalianza Jumapili: ujumbe wa Marekani ulikutana na ule wa ukraine.
Hatua ya pili ilifanyika Jumatatu: mkutano wa Urusi na Marekani. Mjumbe maalum wa Donald Trump nchini Ukraine, Keith Kellogg, alizungumza kuhusu muundo wa mazungumzo wiki iliyopita. "Kutakuwa na mijadala isiyo ya moja kwa moja. Kikundi kimoja kitakuwa katika chumba hiki na kingine katika chumba kingine. Na watashiriki katika mazungumzo - hii ni diplomasia ya ndani ya hoteli moja. Hivi ndivyo itakavyofanyika.
"Tutajua kutoka kwa kila mtu msimamo wake ni upi," Kellogg alisema. Muundo huu pia ulithibitishwa na Rais wa Ukraine. Baada ya mazungumzo ya simu na Trump, Volodymyr Zelensky alisema kuwa hakuna mawasiliano ya moja kwa moja na upande wa Urusi yaliyopangwa.
"Kutakuwa na timu zetu za kiufundi, kama ninavyoelewa, muundo ni kwamba mkutano utakuwa kati ya Ukraine na Marekani. Na kisha Marekani na Urusi. Au hii itakuwa mikutano sambamba na nchi moja juu ya mada moja''.Zelensky alisema.
Mazungumzo ya Jumapili hayatakuwa ya mwisho kwa Ukraine katika hatua hii: wajumbe wa Ukraine, baada ya kufanya mikutano na Wamarekani, hawakuondoka Saudi Arabia na wanasubiri matokeo ya mazungumzo kati ya Moscow na Washington, TASS iliripoti kwa kuinukuu chaneli ya TV ya Ukraine Rada. Habari hii ilithibitishwa Jumatatu jioni na vyanzo vya mtangazaji wa umma wa Ukraine Suspilne katika ujumbe wa Kiukreni.