Masomo katika Chuo Kikuu cha Kenyatta yamesimamishwa kwa muda wa siku tatu zijazo kufuatia ajali mbaya ya barabarani iliyowaua wanafunzi kumi na moja.
Katika taarifa ya siku ya Jumanne, wasimamizi wa taasisi hiyo walisema hatua hiyo inalenga kuwaruhusu kuomboleza wanafunzi waliofariki.
Kusimamishwa kwa masomo kutaanza Jumatano hadi Ijumaa wiki hii.
‘Kufuatia mkasa huu mkubwa, Menejimenti ya chuo kikuu imeamua kusimamisha masomo yote kwa siku tatu kuanzia Jumatano tarehe 20 Machi 2024 ili kutuwezesha kuwaomboleza wanafunzi wetu wapendwa,” taarifa hiyo iliyotiwa saini na msaidizi wa naibu chansela Prof. Waceke Wanjohi ilisoma.
Taasisi hiyo ilifichua kuwa ajali hiyo ilihusisha wanafunzi kutoka idara ya usimamizi wa afya na habari katika Shule ya Sayansi ya Afya.
Ilisema pamoja na wanafunzi kumi na mmoja waliopoteza maisha, wengine kumi na moja walijeruhiwa vibaya huku 16 wakipata majeraha madogo.
"Mipango inafanywa kusafirisha miili ya wanafunzi kumi na mmoja (11) hadi Mochari ya Chuo Kikuu cha Kenyatta kando ya Thika Super Highway," taasisi hiyo ilisema.
Prof Waceke pia alifichua kuwa taasisi hiyo imetenga dawati la usaidizi ili kutoa usaidizi na pia kujibu maswali kuhusu ajali hiyo.
Takriban wanafunzi 11 wa Chuo Kikuu cha Kenyatta walifariki Jumatatu jioni katika ajali mbaya ya barabarani iliyohusisha basi lao la shule na trela, Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Voi Ibrahim Daffala alithibitisha.
Daffala alisema wanafunzi 10 walifariki papo hapo huku mwingine akikata roho hospitalini.
Wanafunzi 42 walipata majeraha mabaya huku wanne wakiwa na majeraha madogo.
"Ajali hiyo ilitokea wakati mvua kubwa ilikuwa ikinyesha. Lori lilijaribu kuondoka kutoka barabarani ili kuepuka mgongano wa uso kwa uso na kusababisha ajali," Daffala alisema.
Picha zilizofikia Radio Jambo zinaonyesha basi la shule liligongwa upande wa kushoto.