Afueni kwa wanaume, mahakama kuu yatoa hukumu watoto chini ya umri wanaweza kulelewa na baba

Muhtasari

• Jaji Joel Ngugi, alielekeza kwamba ingawa dhana ya miaka michanga ni yenye ushawishi katika kuzingatia malezi ya watoto, haiwezi tena kuchukuliwa kuwa kanuni ya sheria isiyobadilika.

• Aliamuru kwamba malezi ya kisheria ya watoto yatashirikiwa kwa pamoja kati ya wanandoa na baba akiwa na malezi halisi/ya kimwili ya watoto hao.

• Pia aliamuru pasipoti za watoto hao ambazo ziko chini ya ulinzi wa mama huyo zikabidhiwe kwa mwanaume mara moja.

Mahakama ya Nakuru ambapo uamuzi wa kihistoria ulioruhusu kulea watoto walio chini ya miaka tisa ulitolewa.
Mahakama ya Nakuru ambapo uamuzi wa kihistoria ulioruhusu kulea watoto walio chini ya miaka tisa ulitolewa.
Image: LOISE MACHARIA

Mahakama kuu ya Nakuru Alhamis ilitoac uamuzi kwamba sasa wanaume wana kila haki ya kuachiwa ulezi wa watoto chini ya miaka tisa na kusema kwamba ulezi wa watoto haifai kabisa kuelekezwa kwa kina mama moja kwa moja kama bado wako chini ya umri.

Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Mkazi, Jaji Joel Ngugi, alielekeza kwamba ingawa dhana ya miaka michanga ni yenye ushawishi katika kuzingatia malezi ya watoto, haiwezi tena kuchukuliwa kuwa kanuni ya sheria isiyobadilika.

Aliongeza kuwa sheria ya mahakama kwamba mtoto wa umri mdogo ni mali ya mama ni matumizi ya kanuni hiyo katika kesi zinazofaa peke yao.

"Sheria ya kisasa huanza na kanuni kwamba mama na baba wa mtoto wote wana haki sawa ya malezi ya mtoto," alisema.

Jaji Ngugi alisema hakuna sababu ya kuzuia malezi ya kisheria kwa mzazi mmoja tu katika hali ambayo hakuna ushahidi kwamba mzazi mmoja hafai au hawezi kuchukua jukumu hilo.

Akitoa uamuzi katika kesi ambapo wanandoa walikuwa wakipigania haki ya kuwalea watoto wao wawili wenye umri wa miaka tisa na 15, Jaji Ngugi alisema dhana ya miaka michanga  sasa lazima izingatiwe kwa maslahi bora ya kanuni za watoto katika kuamua kesi za malezi yao.

Kwa mujibu wa uhalisia wa kesi hiyo mahakamani, wanandoa hao wanadaiwa kufunga ndoa katika Jimbo la Alabama nchini Marekani lakini waliachana rasmi mwaka 2010 kutokana na tofauti zisizoweza kusuluhishwa.

Kufikia wakati wa talaka mnamo Novemba 2010, wanandoa hao walikuwa na mtoto mmoja aliyezaliwa mwaka wa 2007 ambaye malezi yake yalitolewa kwa mama yake na Mahakama ya masuala ya kinyumbani ndani ya Kaunti ya Jefferson, Alabama huku baba yake akipata mapendeleo maalum ya kutembelewa.

Walakini, mapenzi yaliota na kusitawi tena kati ya wanandoa hao tena muda mfupi baada ya talaka yao, walihamia pamoja na mtoto wa pili alizaliwa mnamo 2013.

Wawili hao baadae walirudi nyumbani kwao Kenya ambapo walianzisha biashara ya mgahawa lakini baadae wakakosana tena baada ya mama watoto kuacha biashara hiyo na watoto na kurudi zake Marekani.

Mwanamke huyo alirejea tena Kenya mwaka wa 2021 ambapo alikuwa na nia ya kupata upya visa na stakabadhi za usafiri za watoto wao wawili ili atoroke nao kurudi Amerika, hapo ndipo mwanaume huyo alitafuta huduma ya mahakama ili kuzuia kitendo hicho cha wanawe kuhamishwa kwenda Marekani.

Jaji Ngugi alisema ufaafu wa mama lazima upimwe pamoja na mambo mengine kama vile ukweli kwamba watoto wamekuwa chini ya uangalizi wa baba yao kwa angalau miaka minne iliyopita.

"Jamaa ya watoto wanaishi hapa Kenya. Ikiwa watahamia Marekani, hawatakuwa na ushirikiano wa usaidizi wa kifamilia na uhusiano unaofanyika nchini Kenya,” alisema hakimu huyo.

Jaji Ngugi aliamuru kwamba malezi ya kisheria ya watoto yatashirikiwa kwa pamoja kati ya wanandoa na baba akiwa na malezi halisi/ya kimwili ya watoto hao.

Pia aliamuru pasipoti za watoto hao ambazo ziko chini ya ulinzi wa mama huyo zikabidhiwe kwao mara moja.