Mwanamume akana mashtaka ya kumlawiti mvulana

Muhtasari
  • Alikanusha mashtaka na kuiambia mahakama kuwa alikuwa katika uhusiano wa kimapenzi na mamake mvulana huyo
Image: CLAUSE MASIKA

Mwanamume mmoja Jumatano aliishangaza mahakama ya Kibera baada ya kudai kuwa alilala na mama wa mvulana wa umri wa miaka tisa ambaye anadaiwa kulawiti.

Japheth Kiprotich alifikishwa mbele ya hakimu mkazi wa Kibera William Tullen kujibu shtaka la kumlawiti mvulana wa umri wa miaka tisa.

Alikanusha mashtaka na kuiambia mahakama kuwa alikuwa katika uhusiano wa kimapenzi na mamake mvulana huyo.

"Nililala na mama yake pekee wala si mvulana mdogo kama unavyodai," Kiprotich alisema.

Alitupilia mbali mashtaka hayo akisema ni ya nia mbaya na kuitaka mahakama kutupilia mbali kesi hiyo.

Waendesha mashtaka wa serikali Jane Gitai na Ann Wanjiku hawakupinga kuachiliwa kwa Kiprotich kwa bondi lakini waliitaka mahakama kumpa masharti magumu wakisema kosa hilo ni kubwa.

Karatasi ya mashtaka inasema Kiprotich alitenda kosa hilo mnamo Aprili 30 huko Southlands katika kaunti ndogo ya Lang'ata, Kaunti ya Nairobi.

Inadaiwa alitembelea nyumba ya mtoto huyo na kumshawishi alale sakafuni kabla ya kulawiti.

Mvulana huyo hakuweza kupiga kelele kuomba msaada kwani inasemekana mshitakiwa alikuwa ameziba mdomo wake kwa kitambaa.

Kiprotich pia alikanusha shtaka lingine la kufanya tendo lisilo la adabu na mtoto mdogo. Mahakama ilimwachilia kwa bondi ya Sh300,000 au dhamana mbadala ya Sh100,000.

Kesi hiyo itatajwa Mei 10 kwa ajili ya kusikilizwa mapema.