Kiongozi wa dini ya Kiislamu ameiomba mahakama ya Kenya kutomwachilia huru licha ya kuachiliwa kwa makosa ya ugaidi.
Sheikh Guyo Gorsa Buru alikamatwa Januari 2018 kaskazini mwa Kenya na kushtakiwa kwa kuwa na nyenzo za kulitangaza kundi la kigaidi na kwa kushirikiana na kundi la wanamgambo wa al-Shabab.
Lakini wiki hii, mahakama ilimwachilia ikisema kuwa serikali imeshindwa kuthibitisha kesi yake.
Hata hivyo alikataa kuondoka katika gereza maarufu la Kamiti akisema anahofia maisha yake.
Muhubiri huyo alidai kuwa anaweza kutekwa nyara na kuuawa na serikali mara tu atakapokuwa huru.
Hakimu mkuu aliamuru akae gerezani kwa muda usiozidi siku 30 kisha aachiwe huru.
Hata hivyo atalazimika kuilipa serikali kwa kukaa kwake katika kituo hicho.
Bw Buru amewasilisha kesi tofauti katika mahakama kuu akitaka kupata ulinzi wa serikali pindi atakapoachiliwa.
Kesi yake imeibua mjadala kuhusu watu kutoweka nchini Kenya.
Ripoti ya hivi majuzi ya Amnesty International na mashirika mengine ya kutetea haki za binadamu ililaumu polisi kwa ongezeko la ukatili na mauaji ya kiholela pamoja na utekaji nyara nchini Kenya.
Polisi wamekanusha madai hayo.