Mhubiri ashtakiwa kwa kulaghai mhubiri mwenzake Sh700,000

Muhtasari

•Martin Muraya meshtakiwa kwa kumlaghai Samuel Mburu Sh730,000 akijifanya kuwa na uwezo wa kumuuzia mafuta ya upako.

•Akiwa mbele ya hakimu mkuu wa Milimani Wendy Micheni, Muraya alikanusha mashtaka na kuomba aachiliwe kwa dhamana.

Kanisa
Kanisa
Image: BIBLE STUDY TOOLS

Kasisi mmoja anayefanya kazi mjini Thika ameshtakiwa kwa kulaghai kasisi mwenzake Sh730,000 akijifanya kuwa na uwezo wa kumuuzia mafuta ya upako.

Martin Muraya wa Kanisa la World Victory Church alishtakiwa kwa kupata pesa hizo kutoka kwa kasisi mwenzake, Samwel Mburu Kerige, akidai ana uwezo wa  kusambaza Essential Oil na Seth Molecules.

Mahakama ilisikia kwamba alitenda kosa hilo kati ya Novemba 9 na Novemba 13, 2020, jijini Nairobi, akiwa na nia ya kulaghai.

Kulingana na ripoti ya upande wa mashtaka, wachungaji hao wawili walifanya kazi pamoja hapo awali lakini wakaenda tofauti baada ya mmoja wao kuanzisha kanisa lake.

Kwa vile walikuwa marafiki, Mburu alimwendea Muraya na kumuuliza kama angeweza kusaidia kupata mafuta ya upako kwa ajili ya kanisa lake.

Akiwa mbele ya hakimu mkuu wa Milimani Wendy Micheni, Muraya alikanusha mashtaka na kuomba aachiliwe kwa dhamana.

Aliachiliwa kwa bondi ya Sh500,000. Kesi hiyo itatajwa baada ya wiki mbili.

Wakati huo huo, katika mahakama hiyo, raia wa Sudan Kusini pia alishtakiwa kwa kukaa katika Hoteli ya Serena na kukosa kulipa bili ya Sh359,261.

Amir Ahmed Mohammed alidaiwa kukosa kulip  bili hiyo baada ya kukaa katika hoteli hiyo ya kifahari kati ya Aprili 12 na 28.

Alikuwa ameahidi kulipa ifikapo Aprili 29, lakini alishindwa kutimiza ahadi hiyo.

Mashtaka yalisema alijitwika dhima hiyo kwa nia ya kudanganya.

Alikanusha mashtaka na kuachiliwa kwa dhamana ya pesa taslimu Sh100,000.