Kesi ya mauaji ya ndugu wa Kianjokoma yaahirishwa kufuatia kutokuwepo kwa mwendesha mashtaka

Sasa itasikizwa kuanzia Mei 16.

Muhtasari

•Kesi hiyo ilikuwa isikizwe Jumatatu lakini mahakama iliarifiwa kuwa wakili wa upande wa mashtaka hakuwepo kazini.

•Upande wa mashtaka ulisema watathibitisha kortini kwamba maafisa sita walioshtakiwa walipanga mauaji ya ndugu hao wawili.

Polisi sita walihusishwa na vifo vya ndugu wa Embu katika mahakama ya Millimani mnamo Agosti 17, 2021
Polisi sita walihusishwa na vifo vya ndugu wa Embu katika mahakama ya Millimani mnamo Agosti 17, 2021
Image: MAKTABA

Kesi dhidi ya  maafisa sita wa polisi wanaoshtakiwa kwa mauaji ya ndugu wawili wa Kianjokoma sasa itasikizwa kuanzia Mei 16.

Kesi ya mauaji ya ndugu wa Kianjokoma yaahirishwa

Jaji wa Mahakama Kuu Daniel Ogembo aliahirisha kesi hiyo na kuagiza wahusika kufika kortini Jumatatu wiki ijayo ili kesi hiyo kusikizwa.

Katika kikao cha kusikiliza kesi cha awali kilichofanyika Machi mahakama iliambiwa kaka mkubwa  kati ya wawili walifariki huenda alijitolea maisha yake katika juhudi za kumwokoa mdogo wake kabla ya wote wawili kuuawa.

Chris Dan Murimi, rafiki wa utotoni wa Benson Ndwiga na Emmanuel Ndwiga, ndugu wawili waliopatikana wameuawa baada ya kukamatwa Embu, aliambia mahakama kwamba alimwona Benson akirudi kumuokoa mdogo wake Emmanuel huku polisi waliokuwa na fimbo ndefu wakielekea upande wao.

Murimi alimweleza Jaji Ogembo kwamba yeye, Benson, Emmanuel na rafiki mwingine aliyetambulisha kama John Mugendi walikuwa wakirejea nyumbani mnamo Agosti 1, 2021 walipoiona land cruiser ya polisi.

Benson alikuwa wa kwanza kuliona gari hilo la polisi na kuwapasha wenzake habari.

Muda mfupi baadaye, mahakama ilisikia kwamba afisa wa polisi aliyekuwa amesimama kando ya gari aliwakaribia na wakaamua kukimbia.

“Wakati tulikuwa tunakimbia, Emmanuel alijikwaa, nilitazama nyuma na kumuona akiwa chini. Kisha nikamwona Benson akijizuia, kisha akarudi kule alikokuwa Emmanuel,” Murimi alisema.

Alipoulizwa na wakili Dorcas Mwae kwa nini waliamua kumkimbia afisa huyo wa polisi, Murimi alisema ni kwa sababu aliyekuwa akiwakimbilia "alikuwa mkubwa, kijini na alikuwa akiwakaribia kwa fujo huku akiwa amebeba fimbo kubwa ya mbao".

Alipoulizwa ni kwa nini aliamini kuwa mwanamume aliyekuwa na fimbo alikuwa afisa wa polisi, Murimi alieleza ni kwa sababu alikuwa amesimama kando ya land cruiser.

Aliambia mahakama kuwa madai ya kwamba ndugu hao wawili waliruka kutoka kwa gari la polisi haiwezi kuwa kweli.

Alipotakiwa kufafanua maelezo yake, shahidi huyo alisema kwa sababu ya wahusika wa ndugu huyo, haamini kwamba walikurupuka. "Hawana uwezo wa kuruka nje ya gari la polisi. Najua tabia zao.”

Maafisa walioshtakiwa kwa mauaji ya ndugu hao ni pamoja na Benson Mputhia, Consolata Kariuki, Nicholas Cheruyoit, Martin Wanyama, Lilian Chemuna na James Mwaniki.

Katika maelezo yao ya ufunguzi, upande wa mashtaka ulisema watathibitisha kortini kwamba maafisa hao sita walipanga mauaji ya ndugu hao wawili.