Mwanamke akiri kumdunga mumewe kisu tumboni Eldoret

Muhtasari

•Ruth Chepkurui, 22, alikiri kosa hilo mbele ya Hakimu Mkuu wa Eldoret Dennis Mikoya na kusema alikuwa akijilinda. 

•Mshtakiwa pia aliambia mahakama kuwa alimshambulia mpenzi wake, James Rorman, kwa madai ya kuwa na mahusiano ya kimapenzi nje ya ndoa

Mahakama
Mahakama
Image: MAKTABA

Mwanamke mmoja aliyefikishwa mbele ya mahakama ya Eldoret Jumanne alisimulia jinsi alivyomdunga mumewe tumboni baada ya mzozo wa kinyumbani. 

Ruth Chepkurui, 22, alikiri kosa hilo mbele ya Hakimu Mkuu wa Eldoret Dennis Mikoya na kusema alikuwa akijilinda. 

"Mheshimiwa, ninajuta kilichotokea, na nilikuwa nikijilinda tu kutoka kwa mpenzi mwenye vurugu," alisema. 

Mama huyo wa mtoto mmoja pia aliambia mahakama kuwa alimshambulia mpenzi wake, James Rorman, kwa madai ya kuwa na mahusiano ya kimapenzi nje ya ndoa, jambo ambalo alisema lilimsukuma hadi ukutani na kuzua vurugu. 

Mahakama iliambiwa kuwa mshtakiwa alimvamia mlalamishi usiku wa Mei 26 katika kijiji cha Boma katika Kaunti Ndogo ya Turbo, Kaunti ya Uasin Gishu na kumdhuru vibaya kinyume cha sheria. 

Kulingana na walioshuhudia, wawili hao walipigana kabla ya mwanamke huyo  kuchomoa kisu cha jikoni na kumdunga mpenzi wake. 

Mmoja wa majirani alisema wawili hao wamekuwa wakipigana mara kwa mara nyumbani. 

"Usiku wa tukio, tulisikia zogo baada ya kujua kuwa mshtakiwa alimkabili mumewe baada ya kujua kuwa alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanamke mwingine," alisema mmoja wa majirani zake. 

Mwanamume huyo aliyejeruhiwa alikimbizwa katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Moi, Eldoret, akiwa katika hali mbay na kulazwa kwa siku sita. Aliruhusiwa kuenda nyumbani  mnamo Juni 3. 

Ripoti ya uchunguzi wa kimatibabu kutoka Hospitali ya Moi Teaching & Referral Hospital ilionyesha kuwa alijeruhiwa vibaya.

Mahakama iliamuru maafisa wa uangalizi wa majaribio kufanya uchunguzi wa kijamii kuhusu tabia ya jumla ya mshtakiwa kabla ya hukumu. Kesi hiyo itatajwa Juni 27.