Jamaa taabani kwa kutishia kumnyonga mkewe na kuuchoma mwili wake

Muhtasari

•David Kipng’etich Bett alishtakiwa mbele ya hakimu wa mahakama ya Kibera Jacqueline Muthoni Ojwang na kukanusha mashtaka.

•Kulingana na upande wa mashtaka, mzozo huo ulianza baada ya mshtakiwa kushuku kuwa mkewe alikuwa akitoka kimapenzi na mwanaume mwingine.

David Kipng’etich Bett katika mahakama ya Kibera mnamo Juni 8
David Kipng’etich Bett katika mahakama ya Kibera mnamo Juni 8
Image: CLAUSE MASIKA

Mwanamume aliyetishia kumnyonga mkewe na kuuchoma mwili wake alifikishwa mahakamani siku ya Jumatano.

David Kipng’etich Bett alishtakiwa mbele ya hakimu wa mahakama ya Kibera Jacqueline Muthoni Ojwang na kukanusha mashtaka.

Kulingana na stakabadhi za mashtaka zilizosomwa na karani wa mahakama Evans Koech mshtakiwa alitenda kosa hilo mnamo Mei 15 katika eneo la Amboseli,  kaunti ndogo ya Dagoretti, Kaunti ya Nairobi.

Kipng’etich anadaiwa  kutishia kumuua mkewe Peris Chepkoech .

 "Ulitishia kumnyonga Peris Chepkoech Kuyioni hadi kufa na kuuchoma mwili wake katika nyumba yako ya kupanga," Koech alisema.

Kulingana na upande wa mashtaka, mzozo huo ulianza baada ya mshtakiwa kushuku kuwa mkewe alikuwa akitoka kimapenzi na mwanaume mwingine.

Upande wa mashtaka unasema mshtakiwa aliibua suala hilo kwa mlalamikaji na wakasuluhisha kwa amani kwa ajili ya ndoa na watoto wao.

Hata hivyo, siku hiyo ya tukio, Bett anaripotiwa kumtumia mkewe ujumbe wa kutatanisha akionyesha kwamba angemuua kutokana na pesa alizomtumia kwa ajili ya karo ya shule.

Mshtakiwa alidai maelezo kutoka kwa mkewe kuhusu jinsi alivyotumia pesa.

Karatasi za mahakama zinaonyesha kuwa hapo awali Bett aliwahi kumpiga mlalamishi vibaya kichwani na kujaribu kumkata mkono wake wa kushoto.

Hakimu alimwachilia kwa bondi ya Sh200,000 au dhamana ya pesa taslimu Sh100,000 na mdhamini wa kiasi sawa na hicho.

Aliagiza kesi hiyo itajwe tena Juni 29 kwa maelekezo zaidi.