Mahakama Kuu yasimamisha uamuzi wa CUE kubatilisha shahada ya Sakaja

Muhtasari

•Sakaja alifika kortini Jumatano jioni kusimamisha hatua ya CUE ya kubatilisha utambuzi wa shahada yake.

•Mahakama iliagiza CUE kudumisha uhalali wa shahada ya Sakaja ikisubiri maelekezo zaidi ya mahakama.

Mgombea Ugavana wa Naairobi Johnson Sakaja mbele ya Kamati ya IEBC ya Kusuluhisha Mizozo katika Mahakama ya Milimani mnamo Juni 15 2022.
Mgombea Ugavana wa Naairobi Johnson Sakaja mbele ya Kamati ya IEBC ya Kusuluhisha Mizozo katika Mahakama ya Milimani mnamo Juni 15 2022.
Image: DOUGLAS OKIDY

Mahakama Kuu imesimamisha uamuzi wa Tume ya Elimu ya Vyuo Vikuu (CUE) kubatilisha utambuzi wa shahada ya Seneta Johnson Sakaja.

Mahakama iliagiza CUE kudumisha uhalali wa shahada ya Sakaja ikisubiri maelekezo zaidi ya mahakama.

"Amri ya Certiorari ya kutolewa katika mahakama hii tukufu na kufuta uamuzi wa Tume ya Elimu ya Vyuo Vikuu iliyotolewa tarehe 14 Juni, 2022, kubatilisha kutambuliwa kwa shahada ya mlalamishi (Sakaja) kutoka Chuo Kikuu cha Teams, Kampala, Uganda," mahakama ilisema. kwa sehemu.

Mahakama kuu pia imezuia IEBC kufutilia mbali jina la Sakaja kwenye orodha ya wawaniaji walioidhinishwa kuwania kiti cha ugavana.

Sakaja alifika kortini Jumatano jioni kusimamisha hatua ya CUE ya kubatilisha utambuzi wa shahada yake.

Amri kuu alizotaka mahakamani zote zimetolewa.

CUE ilikuwa imebatilisha utambuzi wa shahada ya Sakaja ikitaja malalamiko mengi.

Barua kutoka kwa Tume ya tarehe 14 Juni, 2022, ilisema ilikuwa imepokea habari muhimu kuhusu uhalisi wa Shahada ya Kwanza ya Sayansi katika Usimamizi.

Tume hiyo ilisema shahada hiyo itachunguzwa zaidi ili kubaini uhalali wake.

"Kwa hivyo, kwa mujibu wa taratibu za utambuzi wa CUE, tunabatilisha utambuzi wa shahada yako kutoka chuo kikuu kilichotajwa," mwenyekiti wa CUE Chacha Nyaigoti Chacha alisema.

Tume hiyo mnamo Juni 6 ilimwandikia seneta huyo barua ikithibitisha kutambuliwa kwa cheti hicho.