Mshukiwa mkuu wa mauaji ya kiholela Nakuru azuiliwa kwa siku 14

Familia za washukiwa 5 waliotajwa na Michori wamejitokeza kukanusha madai ya kuhusika na mauaji hayo.

Muhtasari
  • Hukumu hiyo ilitolewa na Hakimu Mkuu Mwandamizi wa Nakuru Charles Ndegwa na itamfanya Michori kusalia korokoroni hadi uchunguzi wa mauaji hayo utakapokamilika
Mahakama
Mahakama

Evans Michori, mshukiwa mkuu wa visa vingi vya mauaji eneo la Mawanga mjini Nakuru amezuiliwa kwa siku 14.

Hukumu hiyo ilitolewa na Hakimu Mkuu Mwandamizi wa Nakuru Charles Ndegwa na itamfanya Michori kusalia korokoroni hadi uchunguzi wa mauaji hayo utakapokamilika.

Mshukiwa huyo alikamatwa Alhamisi alasiri katika maficho yake huko Keroka, Kaunti ya Kisii.

Baada ya kukamatwa, Michori aliwataja Julius Otieno, 27, Josphat Simiyu, 24, Dennis Mmbolo, 25, Isaac Kinyanjui, 18, na Makhoha Wanjala, 25 kuwa washirika wake.

Afisa wa Upelelezi wa Jinai katika Kaunti ya Nakuru Anthony Sunguti alisema awali washukiwa hao wanaaminika kuhusika na mauaji ya wanawake wanne mjini Nakuru kati ya Desemba 2021 na Juni 2022.

Mauaji hayo yaliwalenga wanawake, ambao miili yao ilipatikana ikiwa imechomwa moto ndani ya nyumba yao. Uhalifu huo unasemekana kutendeka wakati wa mchana.

Familia za washukiwa 5 waliotajwa na Michori wamejitokeza kukanusha madai ya kuhusika na mauaji hayo.